Na Mwandishi wa Malunde 1 blog Dar es salaam
Mwanaume aliyejulikana kwa jina la David Makerege Mluli (80) amekutwa amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Mbezi Garden iliyopo Mbezi jijini Dar es salaam akiwa na mpenzi wake aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kibaya (33).
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni ACP Ramadhan Kingai amesema tukio hilo limetokea Januari 16,2021 majira ya saa 9 alasiri katika eneo la Mbezi Beach ambapo Jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa Meneja wa Hoteli ya Mbezi Beach Garden, Newton Mkonda kuwa katika hoteli hiyo kuna mteja amefariki dunia.
"Baada ya taarifa hiyo kupokelewa, Jeshi la polisi lilifika katika hoteli hiyo chumba namba 22 na kubaini uwepo wa maiti ya mwanaume ambaye baada ya kupekua katika nguo zake vilikutwa vitambulisho vyenye majina ya Davis Makerege Mluli (80) mkazi wa Goba aliyekuwa amekodi chumba hicho",ameeleza
"Pia katika chumba hicho alikutwa mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kibaya (33) mkazi wa Goba ambaye katika maelezo yake alieleza kuwa marehemu alikuwa mpenzi wake", ameongeza Kamanda Kingai.
Ameongeza kuwa mwanamke huyo alieleza alifika hotelini hapo Januari 16, saa tisa na walipokuwa wamekubaliana wakutane na kumkuta marehemu ameshachukua chumba namba 22 akiwa na maji na juice, baada ya kufika aliweza kuagiziwa chips na mishikaki mitatu na mzee huyo.
"Akiwa anasubiria chips hizo huku wakiwa wanaendelea maandalizi ya tendo la ngono ghafla alimwona marehemu akipumua kwa shida ndipo akatoka kwenda mapokezi kuomba msaada, baada ya taarifa wahudumu waliongozana na uongozi wa hoteli walifika na kumkuta mzee huyo haongei na hafanyi chochote huku akiwa ametoa macho.
Uongozi wa hoteli ulibaini kuwa mteja wao amefariki dunia, ndipo Meneja akachukua jukumu la kutujulisha Polisi",amesema.
Kamanda Kingai amesema uchunguzi wa awali ulifanyika na kubaini kuwa mwili wa marehemu hauna jeraha lolote ambapo katika upekuzi marehemu alikutwa na simu aina ya tecno na fedha Sh.37,000/= na kuchukuliwa na askari polisi kupelekwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya uchunguzi na hifadhi.
Aidha amesema mwanamke huyo aliyekutwa chumbani ambamo mwili wa marehemu ulikuwemo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Social Plugin