Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Ndugu, Noely Byamungu amesema wamekamata kiasi cha Tani 4 za maziwa ya unga aina ya Miksimiksi ambayo yameiingia nchini bila vibali kwenye ghala la kiwanda cha kufungasha Maziwa ya unga aina ya Cowbell kilichopo cha Uruwira– Chang’ombe, wilaya ya Temeke kinachomilikiwa na Kampuni ya Hawaii products Supplies Limited.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Ndugu Byamungu amesema walibaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Tasnia ya Maziwa unaofanywa na Kampuni ya Hawaii Products Supplies Limited ambayo iliingiza maziwa hayo nchini bila kupata kibali cha uingizaji wa maziwa ili kukwepa tozo.
Vilevile Ndugu Byamungu amesema katika ukaguzi huo walibaini kilo 3661.2 zimeongezewa muda wa kuisha matumizi kutoka tarehe 24.10.2021 kwakipiga chapa mpya ya tarehe ya mwisho wa matumizi ya bidhaa hizo hadi tarehe 24.8.2022 kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa afya za walaji.
Pia, jumla ya kilo 2592 zitokanazo na ujazo wa makopo yenye ujazo wa gramu 400 kilamoja yamefungashwa upya na kutengeneza boksi (carton) 1440 zenye pakiti ndogondogo 400 kwa kila carton zimepigwa chapa ya tarehe ya mwisho wa matumizi hadi 24.8.2022.
Kutokana na utaratibu huo unaofanywa na kampuni ya Hawaii products Supplies Limited, Bodi ya Maziwa ilisimamisha shughuli zote katika kiwanda hicho baada ya kuona udanganyifu na uvunjaji wa Sheria kwa makusudi.
“ Vitendo hivi havikubaliki, havivumiliki wala kuruhusiwa kwa mujibu wa sheria, hivyo sheria itachukua mkondo wake kwa wahusika” Alisema
Mmiliki wa kampuni ya Hawaii products Supplies Limited Bw. Ahmed Suleiman pamoja Meneja uzalishaji wa Kiwanda Bw. Ahmed Amanzi waliwekwa chini ya ulinzi na uangalizi wa polisi katika kituo cha polisi cha Chang’ombe kwa ajili ya mahojiano na kukamilisha taratibu za kisheria.