Na Dinna Maningo,Tarime
Wananchi katika kijiji cha Nyagisya kata ya Kiore wilayani Tarime mkoani Mara wamelazimika watoto wao kupewa huduma ya Kliniki chini ya mti wa muembe huku wakining'inizwa juu ya mti kupimwa uzito na wajawazito nao wakilazwa juu ya meza,madawati,sakafuni ili kupata huduma za afya.
Malunde 1 blog imefika katika kijiji hicho ili kufahamu sababu za huduma ya Kliniki kutolewa chini ya mti ambapo akina mama wakiwa wamebeba watoto wao pamoja na wajawazito walisema kuwa wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa kijiji hakina zahanati na kwamba huduma hiyo ya kliniki hutolewa mara moja kwa kila mwezi.
Pia walisema kuwa wanaepuka umbali wa kilomita 4 kwenda kupata huduma ya Kliniki katika zahanati ya Mtana kata ya Manga,umbali wa km 12 kwenda zahanati ya Gamasara kata ya Nyandoto na hospitali ya wilaya ya Tarime iliyopo umbali wa km14.
Furaha Joseph mkazi wa kijiji hicho alisema,"mimi ni mmoja wa akina mama tunaoteseka kuitafuta huduma ya afya hatuna zahanati ukiugua,au kwenda kupata huduma ya clinic mpaka ujipange uwe na nauli elfu 3,000 ya pikipiki kwenda Mtana,na 5000 kwenda hospitali ya wilaya kama hauna inabidi utembee kwa miguu inachosha".
Happines Johanes alisema kuwa wanapokwenda kwenye zahanati hizo baadhi ya watoa huduma hukataa kuwapa huduma na kuwataka kwenda zahanati ya Gamasara au hospitali ya wilaya jambo ambalo liliwalazimu kuomba kupewa huduma ya kliniki katika kijiji chao ili kuepuka usumbufu.
"Tukienda Mtana nesi wanatuambia nyie nao mnatusumbua si mjenge zahanati yenu? mnakuja tu kurundikana hapa,ukiwa unaanza kliniki wanakusukuma kwenda hospitali ya wilaya. Tunashukuru serikali yetu ya kijiji ilikaa ikaona ni kwanini tuendelee kuteseka tukaona ni bora huduma ya kliniki tuifanye hapa kwetu hata kama ni chini ya mti inatusaidia kupunguza umbali na gharama za nauli na kauli mbalimbali za kukatisha tamaa", alisema Johanes.
Kutolewa huduma hiyo ya kliniki chini ya mti bado ni changamoto kwa akina mama wenye watoto na wajawazito kwa kuwa mvua ikinyesha hutangatanga kutafuta mahali pakufanyia huduma na kujikinga mvua hali ambayo wakati mwingine watoto kupimwa uzito huku nguo ikifungwa juu ya kenchi kwenye madarasa shule ya msingi Nyagisya na Wajawazito kulala juu ya madawati,meza na sakafuni kupata huduma ya cliniki.
"Mwandishi bahati nzuri umekuja siku ya kliniki na umeshuhudia mwenyewe kwa macho yako,huwa tunapima hapa chini ya mti,mvua ikinyesha tunahangaika pakupima na kujikinga ikinyesha tunaenda ofisi ya kijiji nako wakiwa na vikao vyao tunaondoka tena tunaenda shuleni tunaomba tunapewa darasa lakini sasa hivi wanafunzi wamejaa hakuna madarasa inabidi tusubiri wanafunzi wakienda kupata chakula ndiyo tunaingia kama hakuna mvua tunakaa chini ya mti",alisema.
"Nesi anafunga kikoi juu ya kenchi watoto wanapimwa uzito,kwa wajawazito wanaunganisha madawati au juu ya meza analala anapimwa kuangalia kimo cha mtoto,mlalo,mapigo,kama anacheza huduma anapata zote isipokuwa uzito na wingi wa damu hatupimwi,ofisi ikiwa wazi kuna godoro wananchi tulinunua linawekwa chini ya sakafu mjamzito unalala nesi anapiga magoti chini anakupima,tukiwa nje wanaweka meza mjamzito unalala juu ya meza unapimwa meza tunaazima shuleni",alisema Ester Mwita.
Rhobina Meng'anyi alisema kuwa huduma hiyo wanayoipata chini ya mti ni huruma ya serikali ya kijiji na halmashauri ya wilaya ya Tarime baada ya kuona wajawazito na watoto wanavyoteseka kupata huduma ya Kliniki ambapo Mariam Wambura aliwashukuru wauguzi kuwasogezea huduma karibu licha ya changamoto nyingi wanazozipata lakini hawajakata tamaa kuwasaidia.
Wananchi walisema kuwa adha ya mama na mtoto itapungua endapo ikijengwa zahanati kwani bado kuna huduma hawazipati kiwemo ya mjamzito kutopimwa uzito,baadhi ya vipimo kukosekana ,huduma ya kujifungua na matibabu ya ugonjwa hivyo bado hulazimika kuchapa mwendo kuitafuta huduma ya afya.
Ester Simon alisema"Mama mkwe wangu alikufa njiani akiwa anaenda kujifungua alivuja damu nyingi kutokana na mitikiso ya pikipiki barabara mbuvu alafu umbali mrefu,aliacha watoto sita na mke mwenzangu alipofika hospitali ya wilaya alijifungua lakini mtoto alifariki alizaliwa akiwa kachoka,mama mkewe wangu alifia njiani akienda kujifungua aliacha watoto sita na mimi nawatoto sita wakiugua napata shida sana hakuna zahanati".
Anna Ryoba alisema kuwa ni miongoni mwa wanawake waliojifungulia njiani kutokana na umbali mrefu na kwamba kutokuwepo kwa zahanati bado wanatembea umbali mrefu ambao usababisha baadhi ya wajawazito kujifungulia njiani,naye akiwa miongoni waliojifungulia njiani na wengine kujifungua wakiwa nyumbani jambo linalosababisha wengine kufa na watoto wanauzaliwa kufa kwa kwa kukosa huduma za kitaalamu au wakunga wenye utaalamu wa kuzalisha.
Wanaume nao hawakuwa nyuma kueleza kero zao,Athanas Machera alisema kuwa umbali mrefu wa kwenda kufuata huduma ya afya umekuwa kero kwa watoto wanaoachwa majumbani na wazazi wao kwakuwa ushida njaa bila kula chakula wakisubiri wazazi kufika kuwahudumia,wakati mwingine watoto wadogo wanalazimika kuwasha moto ili kupika chakula jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Thomas Wambura ambaye ni mwendesha pikipiki alisema kuwa wajawazito wengi wanajifungua usiku hivyo wakati mwingine waendesha pikipiki hukataa kuwasafirisha usiku na wale wanaokubali huwatoza gharama kubwa na wengine kucheleweshwa kufikishwa hospitali na hivyo kujifungua njiani na nyumbani na wengine kufariki dunia kwa kukosa huduma.
"Ikiwa usiku gharama ni 30,000/= huku ni porini na ni mbali kuna fisi wengi,unakuta unakaa mbali na umelala na mke wako unapigiwa simu wakati mwingine saa saba za usiku au saa nane,hali hii inawashinda mabodaboda wengi mwingine akikupigia simu unaacha kupokea na wakati huo mgonjwa ana hali mbaya anakosa msaada anazidiwa anaamua kuzaa nyumbani wengine wanakufa,au uchungu unazidi anazalia njiani", alisema Wambura.
Rebeka Samson ni miomgoni mwa wauguzi katika zahanati ya Mtana anayetoa huduma ya kliniki chini ya mti kwenye kijiji cha Nyagiswa alisema kuwa ameamua kutoa huduma hiyo kwa kuwa ni sehemu yake ya kazi licha ya kukutana na changamoto nyingi wakati wa utoaji huduma.
"Huwa tunakuja wauguzi watatu leo niko mwenyewe mmoja anaumwa mwingine yuko masomoni,tunatoa huduma ya kliniki tu kwa watoto na wajawazito inayotolewa mara moja kwa mwezi na tunahudumia wagonjwa zaidi ya 50 kama unavyoona niko peke yangu kila kitu nafanya mimi,napima watoto,wajawazito na huduma ya chanjo.
"Isipokuwa uzito wajawazito hatuwapimi mzani wa kuwapimia ni mkubwa kuusafirisha kutoka zahanati ya Mtana ni mbali unaweza kuharibika,huwa tunawashauri waende kupima Mtana,mazingira si rafiki huwezi jua juu ya mti kuna wadudu gani wabaya,wakati mwingine sisimizi wanatusumbua lakini siwezi kukata tamaa maana naipenda kazi yangu na nijukumu langu kutoa huduma,nikiwa sina nauli ya usafiri inanibidi nikope baadae ofisi yangu unilipa", alisema Samson.
Muuguzi huyo alisema kuwa wakati wa mvua anapata shida kuhamahama kutafuta mahali pakutolea huduma na maeneo ya kutolea huduma siyo mazingira salama lakini hulazimika kufanya hivyo ili kuhakikisha huduma ya kliniki inapatikana kijijini kama njia ya kuwapunguzia umbali lakini wajawazito na watoto hufika kwa wingi kupata huduma.
Kutokana na changamoto ya ukosefu wa zahanati wanakijiji wameamua kuchangishana fedha na nguvu zao kujenga zahanati ambapo wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara aliwaahidi kuwachangia milioni 5 ya kununua Saruji na baadhi ya vifaa vya ujenzi.
Mkuu wa shule ya msingi Nyagisya Egid Kamala alisema kuwa shule ina eneo zaidi ya ekari 50,kutokana na changamoto ya zahanati ilitoa eneo ekari 6 kujengwa zahanati na ekari 13 kujenga shule ya Sekondari.
Athanas Wambura alimpongeza Diwani wa Kata ya Kiore Rhobi John ambaye ni mwanamke kwa madai kuwa tangu kijiji hicho kianzishwe mwaka 1974 licha ya kuongozwa na viongozi mbalimbali wa serikali ya kijiji na Madiwani wa kata hawakuwahi kuhamasisha ujenzi wa zahanati lakini yeye amekuwa Diwani wa kwanza kuhamasisha ujenzi wa zahanati na ujenzi umeanza.
Mjumbe wa Serikali ya kijiji hicho Bruno Maswi alisema kuwa wameamua kusitisha ujenzi wa sekondari kwa kuwa kata hiyo ina sekondari mbili na kugeukia kwenye zahanati kutokana na kero nyingi ikiwemo wajawazito kufukuzwa zahanati ya Mtana na baadhi ya wagonjwa kunyima huduma.
Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Nyagisya ambaye pia ni mwenyekiti wa kitongoji cha Senta Ghati John alisema kuwa sababu za wajawazito na watoto kupata huduma chini ya mti ni kutokana na kuwepo mgogoro kati ya kata yao ya Kiore na kata jirani ya Manga kuliko na zahanati ya Mtana kuwataka kujenga zahanati yao nasiyo kwenda kusongamana kwenye zahanati ya Mtana.
"Tukiwa hatuna vikao na hakuna watu wengi tunaowahudumia tunawaachia ofisi wanawahudumia wajawazito,nawapongeza wananchi kwa kujitolea kuhakikisha tunajenga zahanati wagonjwa na Wajawazito wanateseka sana uongozi wa kijiji tulikaa na uongozi wa shule tukashauriana eneo likapatikana la kujenga zahanati nawaomba wadau mbalimbali waguswe watusaidie tukamilishe ujenzi tumechoka kutukanwa na watu wa Mtana", alisema.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyagisya Waitara Kemo ambaye ana miezi minne tangu ahamishiwe kwenye kijiji hicho alisema kuwa tayali wananchi wamechimba msingi kwa nguvu zao,wamechanga fedha na tripu 5 za mawe zimenunuliwa,matofali 3,500,tripu nne za mchanga,mifuko 30 ya saruji na kuna kiasi cha milioni 1 na vitatumika kuanzia ujenzi na kwamba lazima ujenzi utakamilika ili kusogeza karibu huduma ya afya.
Diwani wa kata ya Kiore Rhobi John alisema kuwa kwakuwa wajawazito na watoto wanateseka sana akiwa kama Diwani wa kwanza mwanamke kuchagulia ndani ya kata hiyo atazidi kuhamasisha ujenzi wa zahanati baada ya kuona wagonjwa,wajawazito na watoto wanavyoteseka nakwamba Zahanati itakamilika mwaka huu na atashirikiana na wananchi wa kata yake katika maendeleo.
Social Plugin