Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (wa pili kushoto) akizungumza na Walimu wa Ufundi wa Shule ya Msingi Makiungua iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida alipoitembelea juzi kwa lengo la kukagua uwezeshwaji mafunzo na ujuzi kwa vijana.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa, Frederick Ndahani ameishauri Serikali kufufua Shule za Msingi za ufundi Nchini.
Ndahani alitoa ushauri huo juzi alipotembelea Shule ya Msingi Makiungu iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa lengo la kukagua uwezeshwaji mafunzo na ujuzi kwa vijana.
Ndahani alisema Shule ya Msingi Makiungu ni moja ya shule zilizofanya vizuri katika mradi waliopewa wa kutengeneza madawati 1000 ya shule za msingi zilizopo wilayani humo.
Ndahani alisema shule hiyo ya mchepuo wa ufundi ni moja ya shule inayoifanya vizuri na kusababisha ofisi ya mkurugenzi wa wilaya ya Ikungi kuwapa kazi ya kutengeneza madawati hayo.
" Shule hizi za mchepuo wa ufundi hapa nchini zikiboreshwa zinaweza kusawaidia vijana wa kitanzania kupata ujuzi wa ufundi mbalimbali." alisema Ndahani.
Alisema wanafunzi wanaojiunga katika shule hiyo hapa ni wale ambao wamekosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari na vyuo na kuwa faida wanayoipata ni kupata mafunzo hayo ya ufundi bure kama ilivyo elimu ya msingi.
Alisema kuboreshwa kwa shule hizo kutasaidia kupata mafundi ambao watatumika kukarabati samani mbalimbali zilizopo mashuleni badala ya kuwapa mafundi kutoka nje ambao watahitaji kulipwa fedha nyingi.
Kwa upande wao Walimu wa Ufundi katika shule hiyo Cosmas Uhiku na Haji Kidabu Wameiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kutosha kwani wanao uwezo wa kuwapatia vijana mafunzo ya kisasa sanjari na vyeti baada ya kumaliza mafunzo kwa muda wa miaka miwili.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Hashimu Ntandu amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kuwapatia mradi huo mkubwa wa kutengeneza madawati ambapo wanatengeneza kwa gharama nafuu.
Social Plugin