Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AWATAKA WAZAZI, MAAFISA USTAWI KUWA KARIBU NA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

 


 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (aliyevaa miwani) akikabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu, Halmashauri ya Ikungi, mkoani Singida.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa kituo hicho Padre Tom Ryan, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.

 Dk. Jingu akifurahi kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa kituo hicho.
 Dk. John Jingu (kushoto) akisalimiana na Diwani wa Siuyu Celestine Yunde, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.
Dk. John Jingu (kulia) akizungumza na watendaji mbalimbali walioshiriki katika hafla hiyo ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.

Na Dotto Mwaibale,  Singida

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu, amewataka wazazi wanaoishi na watoto wenye changamoto za ulemavu wa aina mbalimbali kuwathamini sanjari na kuwapa matunzo stahiki katika malezi na makuzi yao.

Jingu aliyasema hayo alipotembelea na kutoa zawadi za bidhaa mbalimbali na chakula kwa watoto wa Kituo cha Walemavu Siuyu, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani hapa juzi

“Wazazi wawathamini watoto bila kujali hali zao. Kuna baadhi wanawaleta watoto kwenye vituo na kisha kuwatelekeza…hii haikubaliki ni lazima tuzingatie haki za msingi za malezi na makuzi ya watoto hususani watoto hawa wenye ulemavu,” alisema Jingu.

Aidha, aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuongeza kasi ya kuhakikisha wanawatangamanisha watoto na wazazi wao-sambamba na jamii katika muktadha wa kubadili fikra, mtazamo ili kuleta ustawi wa watoto hususan wale wenye aina mbalimbali za ulemavu katika ngazi zote bila kubagua.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, kituo hicho cha Siuyu ni miongoni mwa vituo vyenye sifa stahiki za utoaji wa huduma za malezi kwa watoto, ikiwemo usalama wa kutosha sambamba na walimu waliosomea elimu maalumu ya watoto wenye ulemavu, huku akiwataka viongozi wa vituo vingine nchini kuzingatia matakwa ya kisheria katika uendeshaji wa huduma za usajili wa vituo vyao.

“Moja ya majukumu yetu ni kuvisajili na kuhakikisha vituo hivi vinafanya kazi sawasawa. Hivyo nimekuja hapa kutembelea kituo hiki kwa lengo la kukagua lakini nimeona pia nitoe zawadi kwa watoto hawa ambazo ni bidhaa na chakula,” alisema Jingu.

Hata hivyo, Diwani wa Kata hiyo, Selestine Yunde, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kutembelea kituo hicho huku akimsihi kuangalia namna ya uwezekano wa serikali kuanza kutenga bajeti za kuhudumia vituo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Padre Tom Ryan, alisema ziara ya viongozi wa serikali akiwamo Jingu hutafsiri faraja, ustawi na kuchagiza ustawi na furaha kwa watoto hawa. “Tunaona fahari kwa kutiwa moyo na hamasa kupitia zawadi hizi,” alisema.

Huku mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Raymond Daudi, mbali ya kushukuru, aliomba mamlaka ndani ya serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wenye ulemavu, hususan wahitimu wa darasa la saba kwa kuwatengenezea mazingira ya kujipatia kipato badala ya kuwaacha bila ya msaada wowote.

Awali, akisoma taarifa ya kituo hicho, Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Paul Sangalali, alisema kituo hicho cha Siuyu, kilichopo wilaya ya Ikungi mkoani hapa kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Ulaya na Marekani na kilifunguliwa Februari 2007 na aliyekuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Desderis Rwoma.

Hata hivyo, Sangalali alisema mbali ya mafanikio yaliyopo, kituo kinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhitaji wa baiskeli kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa viungo, uhitaji wa chakula, sabuni, mashuka na fedha kwa ajili ya nauli ya kuwarudisha watoto nyumbani wakati wa likizo.

“Pia miundombinu yake sio rafiki sana hasa pale watoto wanapokuwa wakielekea shule ya msingi Siuyu, na kuna ushirikiano hafifu kwa wazazi kuchangia shilingi laki moja za huduma kwa kila mwaka…lakini watoto wanapokuwa likizo nyumbani hawapati mazoezi kwa wazazi hivyo wakirudi kituoni walimu hulazimika kuanza upya kufundisha,” alisema Sangalali. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com