Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBWA ANG'ATA WATU 15 ...ALETA HOFU YA MLIPUKO WA KICHAA CHA MBWA KIBAHA


Mkazi wa KwaMatiasi Kibaha Mkoani Pwani Abdalah Kidui akionyesha sehemu aliyong'atwa na mbwa anayedhaniwa kuwa na kichaa ambaye pia amewang'ata watu zaidi ya 13 kwa nyakati tofauti mapema katika mtaa wa Mualakani 

Na Julieth Ngarabali - Pwani
Hofu imetanda kwa wakazi wa maeneo ya Kwamatiasi, Jamaika na Mbwate mjini Kibaha baada ya mbwa mmoja ambaye hajajulikana wa nani kuvizia watu nyakati za jioni na kuwang'ata hovyo ambapo kwa kipindi cha siku nane zaidi ya watu 15 wakiwemo watoto wamejeruhiwa sehemu mbalimbali na mnyama huyo.


Wakati hofu ya kung'atwa ikitanda kila mahali mjini humo pia mashaka ya kumudu gharama za matibabu nayo imewakumba baadhi ya familia ambazo ndugu zao wameng'atwa na mbwa huyo ambaye anadaiwa anaweza kuwa na ugonjwa kichaa.

Mkazi wa KwaMatiasi Abdalah Kaduri ( 61) alisema mbwa huyo amemng'ata mapema juzi mguuni saa mbili usiku akirejea nyumbani kwake akitokea kuswali msikitini eneo la barabara ya Nyumbu.

Kaduri amesema ilikua tendo la ghafla na wenzake walipotaka kumpiga mbwa huyo alichoropoka na kukimbia zake na hivyo aliwahishwa zahanati ya jirani kwa huduma ya kwanza.

"Kilichonisikitisha pamoja na kuvuja damu nyingi huduma ya sindano haipatikani kirahisi maana baada ya kutoka kwenye zahanati nilienda kituo cha afya cha binafsi cha Mwembetayari lakini nako niliishia kuoshwa kidonda na kuambiwa niende kituo cha afya Mkoani",amesema Kaduri.

'Nimegundua tatizo la kuumwa na mbwa mwenye kichaa sio la mara kwa mara , ni kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya mlipuko inaweza kukukuta huna hata senti mfukoni na mbaya zaidi matibabu yake ni gharama, sindano moja ni sh, 30,000 na unatakiwa uchome tano, na bima nao haijaweka utaratibu wa haya magonjwa ya mlipuko ya kichaa cha mbwa kutibiwa kwa kadi basi ni tabu tupu",amesema 

Naye Joakim Mzee anasema mjukuu wake Grace alijeruhiwa na mbwa huyo huyo na changamoto waliokutana nayo ni kutopatikana kirahisi kwa sindano ya dawa ya kutibu maambukizi ya mbwa kichaa hali ambayo mtu hulazimika kutumia muda mwingi kuisaka mbali.

Awali Amisa Athumani mama wa mtoto Rahma Alifa (4) aliyeng'atwa na yeye mapema wiki hii amebainisha kuwa hata hajui huko mbele kama mwanaye atamaliza kuchoma sindano tatu alizobakia kutokana na gharama kuwa ni kubwa wengi watashindwa kukamilisha sindano tano ambapo jumla yake ni sh. 150,000.

"Mtoto ameng'atwa mkononi na mgongoni jioni tulienda hospitali ya Mloganzira na huko akasafishwa vidonda na akaandikiwa sindano tano, moja tumelipa sh. 30,000 akachomwa, na ya pili jana tayari, kimbembe sasa hizo zingine sijui kama tutaweza",amesema Amisa

Aidha Matha Josefu bibi wa mtoto Braiton Saini ameiomba Serikali kuangalia upya namna ya kutoa matibabu bure au kwa gharama nafuu zaidi kwa watu wanaong'atwa na mbwa wanaodhaniwa kua kichaa kwa sababu wengi watapoteza maisha kwa kutomudu gharama na pia matukio ya mbwa ni kama magonjwa ya mlipuko tu.

"Yaani huyu akiyeng'atwa ni mjuu wangu, mimi mwenyewe sina kazi na ni mjane jamani sindano tano inatakiwa 150,000 , na hizi haziusiani na kuosha kidonda na dawa za maumivu, gharama ni kubwa na ukizingatia matukio ya mbwa kichaa sio ya kila mara kama ilivyo magonjwa ya malaria, serikali itoe bure au kwa gharama nafuu kila mtu aibumu",amesema bibi huyo.

Naye Elizabert Onesmo anasema mtoto Anjela Nisile (4) pia ni mmoja wa walionusurika kuuawa na mbwa huyo akiwa anacheza na wenzake hivyo ameshauri watoto chini ya miaka mitano na wazee watibiwe bure wanapopata janga kama hilo kwani kundi hilo halifanyi kazi iwe bure kama ilivyo kwa huduma za T.B. (kifua kikuu).

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mualakani ambako watoto watano waliumbwa na mbwa huyu, Eliamini Mgonjwa msako ulifanyika wa kumkamata mbwa huyo lakini hawajafanikiwa na pia haijajulikana ni wanani mpaka sasa, ila tayari taarifa wameshafikisha idara ya mifugo kwa hatua zingine zaidi.

Ofisa Kilimo msaidizi wa Halmashauri ya mji Kibaha Devid Amos amebainisha kuwa wamepokea matukio hayo na kuwatembelea waathirika na kuwashauri wahakikishe wanapata sindano zote tano maana mbwa huyo yawezekana kabisa ana kichaa, Pia walianza kumsaka na bado wanaendelea kumtafuta mbwa huyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com