Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 16 katika eneo la Embu nchini Kenya, anashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini humo kwa tuhuma za kumuua binamu yake ambaye ni mtoto wa miaka minne, Brayden Mutwiri na kunywa damu yake kwa kile kinadhaniwa kuwa kitendo cha utoaji kafara kisha kuutupa mwili wa mtoto huyo mtoni.
Mwanafunzi huyo wa darasa la 8, juzi Jumatano aliwaongoza maofisa wa upelelezi nchini humo hadi katika Mto Thuci ambapo waliukuta mwili wa Mutwiri ukiwa ndani ya mto huo huku ukiwa umeharibika vibaya hata kushindwa kuutambua vizuri kwani umekaa ndani ya maji kwa wiki nzima.
Mutwiri alipotea mwishoni mwa mwezi Desemba, mwaka jana 2020, nyumbani kwao Kavengero, Mbeere Kaskazini.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake walikamatwa Jumatatu na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Siakago kwa mahojiano baada kupatikana kwa taarifa kuwa anahusika na tukio.
Imeelezwa kuwa, baada ya mahojiano, mtuhumiwa aliwaelekeza polisi kwenye mto ambapo mwili wa mtoto huyo waliutupa, baada ya kufika eneo la tukio, waliukuta mwili ukiwa umekwama katikati ya miamba miwili huku ukiwa umeharibika kutokana na kuvimba pamoja na majeraha uliyokuwa nayo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, mjomba wa watoto hao, Nephat Nyaga alisema mtuhumiwa alisimulia jinsi yeye na wenzake walivyomuua mtoto huyo, kunywa damu yake, kisha kutupa mwili wake mtoni.
Aliendelea kueleza kuwa, yeye pamoja na mwenzake walimshawishi mtoto huyo wakati akicheza nyumbani kwao, kisha wakaondoka naye na kumpeleka mtoni ambako walitekeleza unyama huo.
Chifu wa eneo hilo, Charles Njeru akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwamba mtoto huyo alitoweka nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha mwishoni mwa Desemba, mwaka jana na amekuwa akitafutwa na familia yake bila mafanikio.
Njeru aliongeza kuwa, familia ya marehemu itasubiri matokeo ya uchunguzi wa mwili huo ili kubaini chanzo cha kifo na kuthibitisha iwapo mwili huo ni wa mtoto Mutwiri.
Aidha, alisema hicho kimekuwa kisa cha pili cha mtoto aliyepotea na kupatikana akiwa amekufa mtoni. Mtoto mwingine ambaye alikuwa wa kike alipotea na mwili wake ukakutwa mtoni miezi mitatu iliyopita.
Njeru aliwaonya wananchi kutojichukulia sheria mkononi, pia aliwaasa kutokuwa na chuki dhidi ya familia zao, watoto wao kwa kushambulia na kuwaua kwa vigezo vya kafara na kutafuta mali kishirikina, na badala yake kufuata taratibu za kisheria za kutatua mizozo na kutafuta mali. Wananchi wa Embu wamelaani vikali mauaji hayo na kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike ili wauaji wachukuliwe hatua za kisheria.