********************************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema inachukua hatua za maksudi za kulinda nguvu kazi yake dhidi ya majanga, ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ambayo yanaweza kutokea na kuwaathiri wafanyakazi hususan katika kipindi hiki ambacho nchi inajenga uchumi imara wa viwanda.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Ummy Nderianaga, ameyasema hayo wakati akihitimisha mafunzo ya Usalama na Afya kazini yaliyokuwa yakitolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Nderiananga amesema TANESCO ina nafasi muhimu katika kuliwezesha Taifa kufikia agenda yake ya kujenga uchumi wa viwanda ambapo ufanisi wa shirika hilo unategemea uwepo wa wafanyakazi ambao watakuwa salama na wenye afya njema.
“Bila shaka mnatambua umuhimu wenu na Shiriki lenu katika kufanikisha agenda ya nchi yetu ya kuimarisha uchumi kupitia mageuzi ya viwanda ambapo ili kufikia azma hiyo ni lazima kuwe na umeme wa uhakika. Hata hivyo, upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu unategemea uwepo wa watumishi wenye afya njema na wenye ujuzi stahiki kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao,”alisema Naibu Waziri huyo.
Aidha, Nderianga amesema ili jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kuleta maendeleo hususan ujenzi wa miradi mikubwa ya umeme na miradi mingine ziwe na tija ni lazima kuhakikisha kwamba nguvu kazi yake inalindwa ipasavyo.
“Ni kutokana na sababu hii ya msingi ndio maana leo mko hapa ili kupewa nyenzo za kujiepusha na madhara ya ajali na magonjwa yanayoweza kujitokeza katika maeneo yenu ya kazi. Kwasababu hiyo, ninaupongeza uongozi wa Shirika pamoja na OSHA kwakuliona hilo na kuchukua hatua kwa wakati,”aliongeza Naibu Waziri.
Akitoa maelezo ya awali kwa Mgeni Rasmi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ambayo yalijikita katika masuala ya utoaji wa Huduma ya Kwanza mahali pa kazi yalitolewa kwa takribani siku tisa kwa makundi matatu tofauti ya watumishi wa TANESCO ambapo kila kundi lilipata mafunzo hayo kwa siku tatu.
Kwa mujibu wa Mtendaji huyo mkuu wa OSHA zaidi ya watumishi 120 wa TANESCO kutoka katika mikoa mbali mbali hapa nchini wamepatiwa mafunzo ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao katika hali ya usalama na afya.
“Tunafahamu TANESCO mnafanya kazi ambazo ni hatarishi hivyo pamoja na kwamba mna fahamu lakini tumeona kuna umuhimu wa kuendelea kukumbushana ili kuweza kuokoa maisha au kupunguza madhara pale ajali au magonjwa yanapotokea katika sehemu zetu za kazi,” alieleza Mwenda.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt.Phillis Nyimbi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo amesema OSHA imekuwa ikifanya vizuri katika Kanda ya Ziwa hususan katika kutoa miongozo na maelekezo kuhusu masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.
Aidha, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Dativa Mahembe na Elton Mwashala wamebainisha kwamba mafunzo waliyoyapata yataleta tija katika kazi zao za kila siku hususan katika kuokoa maisha au kupunguza athari miongoni mwa wafanyakazi wanaopata ajali au changamoto mbali mbali za kiafya wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Japo mafunzo haya yamefanyika kwa siku tatu tu, kiukweli tumejifunza mambo mengi sana ambayo ni muhimu si tu katika sehemu za kazi lakini pia hata majumbani na mahali pengine,” alisema Dativa Mahembe ambaye ni mshiriki na pia mratibu wa mafunzo hayo.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu) ambayo majukumu yake ya msingi ni pamoja na kufanya ukaguzi wa Usalama na Afya katika sehemu za kazi na kutoa mafunzo mbali mbali yakiwemo ya Huduma ya Kwanza, usalama na afya katika shughuli za ujenzi, usalama na afya katika shughuli za mafuta na gesi, Kozi ya Taifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Uchunguzi wa ajali katika sehemu za kazi na kufanya kazi katika majukwaa (Working at Height).
Social Plugin