NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) kwa ufanisi na utendaji mzuri wa kazi zao kiasi ambacho taifa linatambuliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na shughuli zake kutegemewa na nchi za jirani.
Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema hayo jana katika ziara yake alipotembelea na kujionea shughuli na majukumu ya TMA ofisi kuu za mamlaka hiyo zilizopo Jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, kupokea taarifa ya utendaji na kuzungumza na menejimenti ya TMA.
"...Kwanza niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya, sasa endeleeni kuboresha zaidi. Kimsingi nimefarijika sana kusikia Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agness Kijazi pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) hii ni hatua kubwa. Kutambulika kwa Dkt. Kijazi kimataifa ni sifa kwa taifa letu hivyo nawapongeza sana.
"Nimesikia pia Tanzania, imepewa jukumu na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kusaidia mataifa takribani matano jirani zetu upande wa hali ya hewa hii pia ni sifa kwa taifa letu na kukubalika," alisema Naibu Waziri Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokuwa akizungumza na uongozi wa TMA.
Aliitaka TMA kutambua mchango wa wafanyakazi wanaofanya vizuri na hata kuwapongeza na wale wasiowajibika kuwajibishwa ili kuongeza ari ya utendaji ndani ya mamlaka. Aidha ameitaka TMA kuhakikisha taarifa zao zinasaidia katika ujenzi wa miundombinu nchini na pia kuwa na utaratibu mzuri wa kuziifadhi kisasa ili ziendelee kulisaidia taifa leo na hata hapo baadae zitakapo hitajika.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Kasekenya ameviomba vyombo vyote vya habari nchini kusaidia kusambaza taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa wananchi ili ziweze kuwasaidia wananchi kujua na kufuata ushauri wa mamlaka. Alisema licha ya mamlaka hiyo kuchakata taarifa nzuri za hali ya hewa itakuwa kazi bure kama hazitawafikia wananchi mapema na ama kujihami au kujipanga kulingana na ushauri wa wataalam hao.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agness Kijazi alisema viwango vya utoaji wa taarifa sahihi vya TMA vimeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka na kuishukuru Serikali kuongeza vifaa na wataalam pamoja na kuwaongezea ujuzi kielimu mara kwa mara.
"...Tunaishukuru Serikali kwa kutuwezesha kuanzia vifaa vya kisasa, wafanyakazi pamoja na kutuongezea ujuzi kielimu hii yote ni kutuwezesha kufanya kazi zetu vizuri zaidi. Tuna kuhakikishia tutaendelea kufanya kazi kiufanisi zaidi na kuzingatia maelekezo ya Serikali ili kulisaidia taifa," alisema Dkt. Agness Kijazi.