Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge ametembelea Shule ya Msingi King’ongo iliyopo Manisapaa ya Ubungo kujionea uhalisia leo jioni Januari 18,2021.
Hii ni baada ya Rais Dkt. John Magufuli kuwatumia salamu viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufuatia kubomoka kwa madarasa ya shule hiyo na wanafunzi kukaa chini.
Magufuli amesema hayo leo Januari 18, 2021, akihutubia wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Veta Mkoa wa Kagera na kufungua Shule ya Sekondari ya Ihungo ambayo ilibomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10, mwaka 2016 kisha kujengwa upya na Serikali.
“Kuna shule moja ya Msingi ipo Ubungo Dar es Salaam, inaitwa Barango, ina wanafunzi wengi tu na bado wanakaa chini, madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika DC, RC, Mkurugenzi na mbunge yupo na ni Profesa wa Elimu, na wanakusanya kodi. Naongea nikiwa Kagera nikifika Dar, nisikute wanafunzi wanakaa chini, nitakwenda kukagua mwenyewe, ‘message sent and delivered!’
“Hii ni dhambi kwangu kwamba nilikosea kuwachagua baadhi ya viongozi, ndiyo maana nilipofika hapa sikutaka madarasa ya kuandaliwa nikawa navamia madarasa nikakuta madawati yapo, nikasema Haleluya hongereni sana, lakini hiyo shule ya Ubungo maneno haya wayasikie.
“Namshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao (taarifa ya wanafunzi wa Barango, Ubungo Jijini Dar es Salaam) kuwa wanafunzi wanakaa chini. Viongozi wa kule wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa, hayo sio masuala ya kisiasa, hayo mimi ndiyo napenda kuyajua.
“Ninazungumza nikiwa Kagera lakini nikienda Dar es salaam niyakute madarasa ya Shule ya Barango yamekamilika na Wanafunzi hawakai tena chini, nitaenda kuitembelea Mimi hiyo Shule, kama wananisikia meseji sent na imewafikia.
“Kuna sehemu watu wanafanya kazi lakini wengine wanalala, ndiyo maana DED wa Geita nilimfukuza kazi, ananunua gari la milioni 400 huku watu wanachangishwa madawati, ananunua mpaka mabasi ya kusafirisha wafanyakazi, viongozi tuzitumie vizuri fedha za wananchi,” amesema Magufuli.
Social Plugin