Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA,CHINA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KIUCHUMI

 Na Immaculate Makilika- MAELEZO, Chato
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika masuala ya uchumi kwa sababu uhusiano  na urafiki wa nchi hizi mbili ni wa  muda mrefu.

Hayo yamesemwa jana (Januari 8, 2020), Chato mkoani Geita, wakati Rais Magufuli akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) wa kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga, mradi utakaogharimu shilingi trilioni 3.0677.

Rais Magufuli alisema “Natoa wito kwa kampuni ya CCECC inayojenga kipande hiki cha Mwanza hadi Isaka kijengwe kwa haraka zaidi, lakini niombe Serikali ya China katika kipande kilichobaki cha Isaka hadi Makutopora kama wataweza kutukopesha na sisi tutafurahi sana ili  kiweze kujengwa kwa sababu kitasaidia sana katika kuleta  maendeleo ya nchi yetu na baadae tutaendelea kujenga Tabora, Kigoma na maeneo  mengine.”

Vilevile, Rais Magufuli alisema “Nimemuhakikishia Waziri Wang Yi kuwa kufanya biashara na Tanzania kuna faida kwani kupitia nchi yetu watakuwa na uwezo kufanya biashara na nchi zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizo Kusini mwa Afrika kwa sababu Tanzania  ni mwanachama wa Jumuiya hizo”

Alibainisha kuwa China ni nchi tajiri duniani na  Tanzania kuna mazao mengi ambayo yanaweza kuuzwa nchini humo hivyo kuwataka watanzania kutumia fursa huyo kwa kuuza mazao na bidhaa nchini China.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema kuwa amepokea ujumbe kutoka China, lakini pia  ametuma ujumbe kwa  Rais wa China, Xi Jinping kumuomba aisaidie Tanzania katika ujenzi wa miradi ya kufua umeme wa maji mkoani Njombe, Lumakali na Luhuji pamoja na ujenzi wa kilometa 148 za barabara kwa kiwango cha lami Zanzibar.

Fauku ya hayo, Rais Magufuli ametaja baadhi ya  masuala waliyozungumza na Waziri Wang kuwa ni kuomba Tanzania isamehewe madeni iliyokopa  ikiwemo la dola za Marekani milioni 15.7 za ujenzi wa reli ya TAZARA, deni la dola za Marekani milioni 137 la nyumba za askari ambapo Serikali imeshalipa tayari dola za Marekani 164 pamoja na deni la kiwanda cha Urafiki la dola za Marekani milioni 15.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi alisema kuwa uwepo wa Rais Magufuli katika tukio hilo la utiaji saini wa mkataba huo unaonesha umuhimu mkubwa ambao Rais anaupa ushirikiano na urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili na kuzitataka kampuni za kichina kufanyakazi kwa ubora.

“Natumia fursa hii kuyaagiza makampuni ya China yanayotekeleza miradi hapa nchini Tanzania kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia kwanza maslahi ya Tanzania.” Alisema Waziri Wang

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema kuwa zilijitokeza kampuni zaidi ya 18 za kimataifa kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa kipande cha Mwanza – Isaka, baada ya kufanya mchakato kampuni za CCECC zilishinda zabuni, gharama ya mradi ni shilingi trilioni 3.0677.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CCECC, Mhandisi Jiang Yigao alisema kampuni yake imekuwa ikifanyakazi nchini Tanzania kwa zaidi ya  miaka 50 na katika kipindi cha miaka 10 iliyopita imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo daraja la Busisi- Kigongo, Ubungo interchange na ujenzi wa reli ya TAZARA.

“Kama tulivyofanya ujenzi wa TAZARA tutafanya hivyo hivyo kwa kujenga reli hii ya kisasa tukitumia raslimali zilizopo na kujenga mradi huu kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa.” Alisema Mhandisi Yigao

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com