Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TITO MAGOTI NA MWENZAKE WAHUKUMIWA KULIPA FIDIA

 


Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, leo wameachiwa huru na kukubali kulipa faini ya milioni 17, baada ya kukamatwa Desemba 2019 na kufunguliwa mashtaka matatu ikiwemo la utakatishaji wa fedha.

Hukumu hiyo imetolewa leo Januari 5, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega, baada ya washtakiwa hao kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania( DPP), ambapo mbali na faini hiyo, mahakama pia imewahukumu adhabu ya kutokutenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo Januari 5, 2021.

Awali, jopo la mawakili wawili wa upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, akishirikiana na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ulidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya uamuzi baada ya washtakiwa kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP).

Wakili Kadushi ameongeza kuwa washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, lakini baada ya kufanya majadiliano na DPP walifutiwa mawili na kubakisha shitaka moja ambalo ni kuongoza genge la uhalifu.

Katika kesi ya msingi Tito na Theodory, pamoja na wenzao ambao hawakufikishwa mahakamani wanadaiwa kati ya Februari mosi na Desemba 17, 2019, jijini Dar es Salaam na katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, kwa makusudi walishiriki makosa ya uhalifu wa kupanga kwa kumiliki programu za kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu na kupelekea kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 17.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa washtakiwa hao, Flugence Massawe, Jebra Kambole na Pacience Mlowe waliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu kwa sababu ni vijana wadogo na wanategemewa na familia zao.

Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 24, 2019, na kufunguliwa mashtaka matatu, ikiwemo la kushiriki genge la uhalifu, kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa kwa lengo la kutenda uhalifu na utakatishaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 17.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com