UZINDUZI KIJANISHA WILAYA YA IKUNGI-SINGIDA YASHIKA KASI

 

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akiongoza zoezi la maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti kitaifa kwa ngazi ya wilaya mkoani Singida hivi karibuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akishiriki zoezi hilo kikamilifu.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (kulia)na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa pamoja wakiwajibika kwenye maadhimisho hayo.

Mkuu wa Idara ya Usafishaji na Mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Onesmo Rwehumbiza akipanda mti.

Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi Yahaya Njiku na Kamanda wa Jeshi la Akiba wilaya ya Ikungi Massawe wakishiriki zoezi hilo.
Askari wa Jeshi la Akiba wakisikiliza hotuba ya DC Mpogolo kabla ya kuanza zoezi la kupanda miti kwenye maadhimisho hayo.
Watumishi wa Vitengo na Idara mbalimbali wakisikiliza hotuba ya DC Mpogolo kabla ya kuanza zoezi la kupanda miti kwenye maadhimisho hayo .
Maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti yakiendelea.
Maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti yakiendelea.
Maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti yakiendelea.
Kazi ikiendelea.
Kazi ikiendelea.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Ikungi akishiriki ipasavyo zoezi hilo..
Mhifadhi Misitu wa TFS kutoka Wilaya ya Ikungi, Wilson Pikoloti akishiriki maadhimisho hayo.

Mwonekano wa mradi wa ujenzi unaoendelea wa Majengo ya itakayokuwa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Afisa Tarafa wa Ikungi, Josephina Kadaso, akishiriki kupanda miti.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani hapa, Edward Mpogolo ameongoza mamia ya watumishi katika maadhimisho ya uzinduzi wa upandaji miti kiwilaya, ikiwa ni safari ya mwendelezo wa shabaha iliyopo ya hitaji la kufikisha idadi ya miti isiyopungua 709,000, huku kila kaya ikitarajia kupanda miti 10 kwa msimu wa 2020/2021.

Katika uzinduzi huo uliofanyika hivi karibuni, jumla ya miche ya miti 400 ilipandwa eneo la kijiji cha Muungano, mahali unapotekelezwa mradi wa ujenzi wa majengo ya itakayokuwa hospitali ya Wilaya ya Ikungi, huku miti mingine takribani elfu 30 inayozalishwa na TFS ikitarajiwa kusambazwa na kupandwa kwenye taasisi nyingine zote ndani ya wilaya hiyo.

“Shabaha yetu kwa mwaka huu kwanza ni kupanda zaidi ya miche laki saba lakini pia tunatarajia kupanda zaidi ya miche ya korosho milioni moja. Na kuhusu miche ya korosho tayari Jeshi la Kujenga Taifa hapa wilayani wameshazalisha zaidi ya miche laki 3…kikubwa tuendelee kuhamasishana,” alisema Mpogolo

Aidha, aliwataka wakazi wanaoishi ndani ya wilaya hiyo kuhakikisha idadi iliyopangwa ya kupanda miti 10 kwa kila kaya inatekelezwa kikamilifu kwa kiwango cha kuchanganya aina mbalimbali za miti ikiwemo ile ya mbao, lakini bila kusahau kupanda nje ya nyumba zao miti ya kivuli, miembe, korosho na palachichi.

Hata hivyo, aliwataka TFS kuongeza idadi ya uzalishaji miche kutoka elfu 30 iliyopo kwa sasa na kufikia angalau elfu 50 ili kukidhi hitaji la miti hiyo kwa kuzingatia jiografia ya ukubwa wa maeneo yanayozunguka wilaya hiyo ikiwa ni kubariki jitihada zinazoendelea katika kukabiliana na ukame.

“Kwa mwaka huu sitarajii tena kuona kuna upotevu wa miti, nikuombe Mkurugenzi tusimamie kikamilifu sheria zetu ndogondogo ili kutunza hii miti ambayo tumeanza kuipanda leo na tutakayoendelea kuipanda kwa mwaka mzima. Msiruhusu mifugo iwe sababu ya upotevu wa miti yetu,” alisema Mpogolo na kuongeza:

“Tumeamua kufanya uzinduzi huu kwenye hospitali hii sababu tunataka wagonjwa wetu wanapofika hapa wapumzike vizuri na wapate kivuli na hewa safi. Rais John Magufuli ametupatia jumla ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo haya ya hospitali yetu ya wilaya…tunataka siku akija kuizindua basi akute kuna mazingira rafiki na uoto wa miti ya kutosha.”

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya aliagiza kuhakikisha wale wote waliovamia maeneo ya misitu ya Minyughe na Mlilii wanaondoka mara moja ili kuokoa bionuai za misitu hiyo iliyopo ndani ya wilaya ya Ikungi, ambayo siku hadi siku imeendelea kuathiriwa na uvamizi huo unaenda sambamba na shughuli za kibinadamu.

“Kwa bahati nzuri TFS kwa kushirikiana na Halmashauri wameanza kutenga baadhi ya maeneo na tumeshaanza kuangalia athari zilizojitokeza kwenye misitu hiyo ili kukamilisha taratibu zote kuwezesha msitu kupimwa na kupata GN ili tuweze kuumiliki kisheria,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi Justice Kijazi alisema uoto wan chi yetu ni kitu muhimu na ili tuweze kurithisha uoto huo kwenye kizazi kinachokuja tunapaswa kutengeneza mazingira mazuri ya upandaji miti kama zoezi endelevu kwa mfano wa tukio la uzinduzi huo.

Alisema kwa Halmashauri ya Ikungi kuanzia mwaka 2016/2020 imefanikiwa kupanda miti 1,385,900 lakini kati ya hiyo iliyopona mpaka sasa ni 145,860 sawa na asilimia 63.

“Tatizo kubwa linalosababisha uharibifu wa miti inayopandwa ni mifugo inayozunguka kwenye maeneo yetu. Natambua mifugo ni neema lakini wengi wetu tunaifuga kiholela,” alisema Kijazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Usafishaji na Mazingira, Halmashauri ya Ikungi, Onesmo Rwehumbiza, alimweleza Mkuu wa Wilaya kwamba kuna misitu miwili ya asili ya Hifadhi, yaani Miili na Minyughe, lakini misitu hii kwa sasa imevamiwa na watu zaidi ya 1200 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya ikungi.

“Pamoja na halmashauri ya wilaya kujitahidi kuweka mabango ya kukataza mtu yeyote kuingia kwenye hifadhi hizo lakini bado wananchi wanakaidi agizo hilo kwa kuendelea kuingia hifadhini na kufanya uharibifu mkubwa kwenye misitu hiyo ya asili,” alisema Rwehumbiza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post