Mkurugenzi wa taasisi inayohudumia jamii ya WhoisHussein Fatema Kermaili akifungua bomba la maji kuwahakikishia wanakijiji wa Buyuni Chalinze waliokuwa wakitumia maji ya malambo kuwa kisima kilichochimbwa na taaisis hiyo kipo tayari kutumika kwa maji safi na salama.
Kushoto ni Mkurugenzi wa taasisi inayohudumia jamii ya WhoisHussein Fatema Kermaili akionyesha majukumu ya taasisi hiyo kwa jamii ikiwemo mambo ambayo wameshayatekeleza katika maeneo mbalimbali, kulia ni mwenyeji wa taasisi hiyo Vigwaza Mohsin Bharwan.
Na Julieth Ngarabali ,Chalinze.
Tatizo la kusaka maji Safi lililokuwa linawakabili zaidi ya wanakijiji elfu tano (5000) wa Buyuni kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani limemalizwa na taasisi inayotumikia jamii ya WhoisHussein ambayo imejenga na kukabidhi kisima kikubwa katika eneo hilo.
Kisima hicho chenye thamani ya sh. Milioni . 30 kina urefu wa mita za ujao 160 na kwamba kitakuwa kinaendeshwa kwa mionzi ya jua huku ikinufaisha pia wakazi wa vitongoji tisa vya jirani ikiwemo shule za msingi.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo Fatema Kermaili , amekabidhi kisima na kuwataka wanakiji hao kuhakikisha wanatunza kisima hicho ili kiwe chanzo cha kudumu cha maji safi na salama kijijini humo.
Kermaili amebainisha kuwa wameamua kusogeza huduma ya maji katika Kijiji hicho baada ya kukutana ana kwa ana na baadhi ya akina mama na watoto wakichota maji machafu kwenye madimbwi barabarani yaliyotokana na mvua wakati wao wakiwa safarini eneo hilo , hali ambayo waliona wanaweza kupatwa na magonjwa ya matumbo.
"Tukiwa tunatoka katika shughuli zetu za kijamii mvua ikinyesha,tulishuhudia akina mama na baadhi ya watoto wakichota maji machafu ya vumbi yaliyokuwa yakitiririka barabarani na mengine ya kwenye madimbi nikampigia simu diwani wa hapa akaniambia tatizo lipo kubwa tu hivyo tukaamua kujenga kisima hiki waepukana na magonjwa ya mlipuko "amesema Kermaili
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao,mkazi wa eneo hilo Asha Omary amesema walikuwa wanafuata maji mbali kitongoji cha jirani na walitumia saa mbili kutembea hivyo mradi huo umewapunguzia adha hiyo.
"Tunashuru hii taasisi ya WHOISHUSSEIN maana kwa sasa tunakinga maji safi ya bomba tunaachana na yale kwenye malambo ambayo kiukweli hayakuwa salama maana wakati mwingine mifugo nayo inatumia, tunaepuka sasa baadhi ya magonjwa hasa ya matumbo",amesema Asha.
Naye Ashura Ramadhan mwanafunzi wa darasa la Saba shule ya msingi Buyuni amesema pamoja na kuepuka magonjwa yatokanayo na maji machafu pia wataepuka adhabu ya viboko walivyokuwa wanapata kwa kuchelewa kusaka maji mbali kwenye malambo ambayo hata hivyo wakati mwingine yalichafuliwa na mifugo na kulazimika kusubiri yawe masafi ndiyo wachote.
Kijiji cha Buyuni kipo kata ya Vigwaza na kina wakazi 5.007 pamoja na vitongoji tisa , na kwamba chanzo kikuu cha maji walikuwa wakipata kwenye malambo ambayo wakati mwingine mifugo nayo huingia humo na pia waliishi kwa kuvizia maji ya mvua vyanzo ambavyo si salama kiafya.