Mbunge Waitara akisaini kitabu cha mahudhurio baada ya kuwasili kwenye mkutano wa kata ya Sirari. Kushoto ni katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka
Mkutano wa mbunge Waitara uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari
Mkutano wa mbunge Waitara uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari
Mkutano wa mbunge Waitara uliofanyika uwanja wa Tarafa Sirari
Na Dinna Maningo,Tarime
Wananchi wa kata ya Sirari wamesema kuwa kinachosababisha wafanyabiashara kuingiza bidhaa nchini kwa njia za Magendo badala ya kupitisha katika mipaka halali ukiwemo mpaka wa Sirari ni kutokana na ushuru mkubwa wa bidhaa zitokazo nchi jirani ya Kenya ikiwemo Saruji,Sukari na Mafuta ya chakula.
Ili kupunguza tatizo la bidhaa za Kenya kuingia nchini kwa njia za panya,wananchi wameiomba Serikali kushusha bei ya Saruji ya Kenya ili iwe rafiki kwa wafanyabiashara ikizingatiwa kwamba wilaya ya Tarime imepakana na nchi ya Kenya na Saruji ya Tanzania ni gharama ikilinganishwa na ya nchi hiyo jirani.
Wananchi walieleza hayo kwa Mbunge wao wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira,alipokuwa kwenye ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na kisha kuzungumza na wananchi katika uwanja wa Tarafa kufahamu kero zinazowakabili ili zitatuliwe.
Diwani wa kata ya Sirari Amos Sagara (CCM) alisema kuwa wananchi hawakwepi kulipa kodi ila kinachosababisha wapitishe bidhaa kwa njia za panya wanakwepa ushuru mkubwa kwa kuwa unawaumiza kibiashara.
"Saruji ya Tanzania mfuko mmoja unauzwa sh.22,000 bado usafiri na wakati mwingine upatikanaji wake ni wa shida, Boda ya Kenya Saruji inauzwa kwa sh.12,000-13,000 ikiingia Tarime inauzwa sh 17,000 na upatikanaji wake ni rahisi ukichukua ya Kenya kila mfuko unaokoa sh.5,000,cha kushangaza ukipitisha saruji mpakani Saruji ya Kenya mfuko mmoja unatozwa kodi sh.8,500 ndiyo maana wanakwepa",alisema Chacha.
Bhoke Marwa alisema"Mnunuzi anaangalia unafuu wa bei, tunaomba Serikali ishushe bei bidhaa zake kwani ushuru ni mkubwa matokeo yake wananchi nao wanabuni njia za kuingiza bidhaa kukwepa ushuru mkubwa".
Wananchi wanaiomba Serikali kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakuwa na bei nafuu na zipatikane kwa urahisi hususani kwenye wilaya zinazopakana na nchi za jirani kwa kufanya hivyo itasaidia wananchi kupenda na kununua bidhaa za ndani badala ya kwenda kununua bidhaa za nchi jirani kwa sababu ya unafuu wa bei na itasaidia kupunguza uingizaji wa bidhaa za nje kwa njia ya magendo.
Mbunge Waitara alisema kuwa Saruji imekuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi wilayani Tarime hivyo kuna haja ya kulitizama suala hilo kwa mapana zaidi kwa kuwa linawaumiza wananchi na kuahidi kulifikisha mamlaka husika ili litatuliwe.
Mbali na suala hilo wananchi waliomba kuwepo kwa mnada wa ng'ombe ,na wengine kulalamikia vitendo vya uonevu kwa askari wa usalama barabarani,lakini pia Waitara aliwasisitiza viongozi wakiwemo Madiwani kufanya mikutano ya wananchi na kusikiliza kero zao pamoja na ushirikishwaji wa miradi ya maendeleo.