WAZIRI BITEKO AKAGUA WAUZA MADINI DAR, AONYA MATAPELI


Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewacharukia matapeli wanaojihusisha biashara ya uuzaji na ununuzi wa madini kinyemela  majumbani mwao na kuikosesha serikali mapato na kuongeza kuwa huo ni uhalifu ambao kamwe  hautavumiliwa.

Waziri Biteko pia amewaonya matapeli wanaowalaghai wageni kutoka nje ya nchi na kuwauzia madini feki jambo alilosema linachafua sifa ya nchi.

Waziri Biteko ametoa kauli hiyo leo alipotembelea na kuwakagua wafanyabiashara wa madini kwenye soko la madini lililopo Jengo la NHC Barabara ya Samora jijini Dar ambapo alisikiliza changamoto zinazowakabili wadau hao na kuahidi kuzitatua haraka.

 “Lengo letu ni kudhibiti utoroshaji wa madini ndio maana tumekuja kuwapa tahadhari kuwa wajiepushe kununua nje ya mfumo wa masoko kwani madhara yake ni makubwa. ukikutwa unanunua au unauza madini nyumbani kwako hata kama upo kwenye gorofa ya 12, fensi kali na kamera za CCTV tutakukamata.

“Lazima tufuate sheria kwa sababu asilimia saba ya pato hilo sio kubwa kiasi cha kukusababishia kwanza tutaifishe madini, nyumba na hata wewe mhusika kupelekwa ndani,” alisema.

Alisema katika kudhibiti mnyororo wa sekta ya madini, Serikali kupitia wizara ya madini pamoja na wizara ya viwanda na biashara inaandaa muswada wa sheria utakaowawezesha masonara wote nchini kutambulika kisheria.

“Tatizo ni kubwa kwa masonara ni kutotambulika… kwa kuwa wapo wengin hata kuwatambua ni ngumu. Tunataka kuweka msukumo mkubwa zaidi katika udhibiti mifumo mingi katika sekta ya madini na sasa tumeweka mazingira rafiki kwa sababu lengo letu ni uongezaji thamani. Kikubwa nawaomba masonara wawe na subira katika hili,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti Chama cha Wafanyabiashara Wakubwa Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (TAMIDA), Osman Tharia aliiomba wizara kuuangalia upya bei ya pango la vizimba walivyokodishwa na Shirika hilo la nyumba sambamba na bei za umeme kwa kuwa zinawakwamisha katika kukuza biashara ya madini nchini.

“Alisema wafanyabiashara zaidi ya 57 waliopo katika vizimba hivyo hulazimika kulipia umeme kulingana na ukubwa wa kizimba jambo ambalo ni gharama kubwa kwani ilitakiwa kulipia kulingana na matumizi ya umeme,” alisema

Aidha, Naibu waziri wa madini, Prof. Shukrani Manya aliwataka wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria kwa kuwa serikali haina nia ya kuwadhoofisha kibiashara bali inataka kuwawezesha kukua na kufanya biashara ya madini kuwa endelevu na yenye tija kwa pande zote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post