Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJERUHIWA AJALI YA TRENI WARUHUSIWA WOTE


MWANDISHI WETU
Majeruhi 66 waliopata ajali ya treni iliyotokea mwishoni mwa wiki (Januari 2, 2021) wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka hospitali kutokana na  hali zao kuimarika mara baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe Jenista Mhagama ametembelea Januari 4, 2021 na kuwajulia hali majeruhi hao waliokuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali hiyo ambapo hadi sasa wameruhusiwa wajeruhi wote.

Waziri alionesha kufurahishwa na huduma zilizotolewa kwa majeruhi hao na kupongeza jitihada zilizofanyika katika kuokoa maisha yao.

Alielezea kuwa, Serikali imefanya Uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya,na hivyo kuwezesha kutoa huduma kwa namna bora na weledi wenye  kwendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Akiwa wodini hapo waziri alipata fursa ya kuzungumza na majeruhi na kuwaeleza adhima ya Serikali ni kuona inaendelea kuratibu na kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo ya barabara na afya ili pindi zinapotokea ajali kama hizo kuona jamii haipatwi na madhara makubwa kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki inayosaidia kuondokana na madhara ya majanga.

“Kipekee ninawapa pole wale wote waliopatwa na ajali hii  iliyosababisha vifo na majeraha kwa wengine. Serikali imeguswa na ajali hili na tuwaaahidi tupo pamoja na tutaendelea kuhakikisha huduma zetu zinatolewa kwa ubora na wakati,” alisema Waziri

Waziri alieleza kuwa, Serikali kupitia Idara ya Uratibu wa Maafa itaendelea kuweka mikakati thabiti katika kuhakikisha inakuwa na mipango madhubuti ili kuyakabili majanga mbalimbali pindi yanapotokea katika kuokoa maisha ya wananchi na mali zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe, Gerald Maganga alimshukuru Waziri kwa ziara hiyo na kupongeza shirika la Reli kwa namna walivyosaidia katika kuhakikisha walionusurika wanaendelea na safari zao.

“Niwapongeze watendaji wa shirika la Reli walivyoshiriki kwa kuhakikisha kunakuwa na mabasi yanayotoa huduma kwa abiria walionusurika na ajali hii kwa kupatiwa usafiri na kuendelea na safari zao bila usumbufu wowote,”alisema Bw. Maganga

Naye mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Bw. Stephano Kasole alieleza furaha yake kuhusu huduma bora zilizotolewa na hospitali hiyo na kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu muhimu katika sekta ya afya.

“Tumepokelewa vizuri na kupatiwa huduma kwa wakati, hii imechangia kupata nafuu mapema sana, na leo nimefarijika kwa kuwa nimeruhusiwa kutoka,”alisema Kasole

AWALI

Treni ya abiria ilipata ajali tarehe 02 Januari, 2021 ilikuwa imebeba abiria 720 iliyokuwa safarini kutoka Jijini Dar es Salaam ikielekea maeneo ya Tabora, Katavi (Mpanda), Kigoma na Mwanza ilipata ajali kutokana na mvua zilizonyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu na kupelekea kusobwa kwa tuta la njia ya reli.Ajali ilisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 66.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com