Na Dinna Maningo,TARIME
BARAZA la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara wameidhinisha nakupitisha bajeti sh.Bilioni 38,273,963,588.36/= kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo kiwango cha makusanyo kimepanda kwa asilimia tisa ikilinganishwa na sh.Bilioni 34,825,488,137.00/= zilizokisiwa kukusanywa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 huku mapato ya ndani yakiwa yameongezeka kwa asilimia 15.
Katika bajeti hiyo Juzi, Madiwani walipitisha bajeti ya sh Mil.185 ili kulipa deni linalodaiwa na Bohari ya dawa (MSD ) ambalo limesababisha halmashauri hiyo kutopatiwa dawa na hivyo kuwepo kwa uhaba wa dawa kwenye zahanati,vituo vya afya na hospitali ya halmashauri.
Pia halmashauri hiyo imesema itanunua dawa kupitia fedha za mfuko wa kuendeleza jamii katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo unaomilikiwa na kampuni ya Barrick (CSR) sh.Mil. 200 ambao uchangia kati ya Bilioni 4 - 5 kama mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi.
Wakichangia hoja kuhusu ukosefu wa dawa unavyowatesa wagonjwa licha yakulipa gharama za matibabu walisema kuwa wamelazimika kupitisha bajeti kulipa deni hilo ili kuondokana na changamoto ya dawa.
Diwani wa kata ya Komaswa Chacha Baltazari alisema deni hilo lilipwe haraka na kwamba kuchelewa kulilipa kumesababisha wagonjwa wasumbuke kutafuta dawa kwa gharama kubwa kwenye maduka binafsi ya dawa.
Diwani wa kata ya Binagi Marwa Marigiri alisema"kwenye kulipa dawa sisi hatuna ubishi kwasababu kwenye kata zetu tuna huduma za afya ila naomba deni hilo linalolipwa liguse zahanati na vituo vyote vya afya isiwe tu kwenye hospitali ya halmashauri na watumishi wa afya waajiliwe'.
Diwani wa viti maalumu Mariam Mkono alisema kuwa hospitali ya halmashauri ya wilaya haipaswi kutokuwa na dawa kwa kuwa kuna baadhi ya wagonjwa wanaotoka kwenye zahanati na vituo vya afya ambao hupatiwa rufaa kwenda hospitali hiyo wanapokosa huduma kwa sababu ya ukosefu wa dawa kitendo hicho kinawakera.
"Niombe mkurugenzi mtafute fedha za kununua dawa kwa wagonjwa wanaotoka nje ya kijiji cha Nyamwaga ambako kuna hospitali ya halmashauri hiyo hospitali siyo ya kijiji wakati tunasubiri fedha ziende MSD tafuteni fedha za kununua dawa." alisema.
Diwani wa kata ya Kemambo Rashid Bogomba aliongeza"vituo vya afya na zahanati vinadaiwa fedha za dawa naomba vile vituo vyenye fedha kidogo wanunue dawa,dawa bado ni pungufu sana,serikali haipeleki fedha za kununua dawa kwenye vituo,vituo na zahanati ndiyo vinakusanya pesa na kununua dawa suala la upatikanaji wa dawa imekuwa ni shida"
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Peter Nyanja alisema kuwa halmashauri itanunua dawa kupitia mfuko wa CSR kwa ajili ya hospitali ya halmashauri na kuajili wataalamu wa afya kupitia fedha za mfuko huo na aliwashukuru madiwani kwa kupitisha bajeti.
"Tutanunua dawa za sh.milioni 200 kutoka kwenye mfuko wa CSR kwa ajili ya kununua dawa katika hospitali ya halmashauri na kuajili wataalamu wa afya katika vitengo muhimu kama upasuaji,na deni la sh Mil.185 tunalodaiwa na MSD ni madeni kutoka katika hospitali ya halmashauri,vituo vya afya 8 na zahanati 41", alisema Nyanja.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga Simion Samwel aliwashukuru madiwani kwa kukubali kupitisha bajeti ya kulipa deni la MSD ambalo limesababisha Halmashauri kutopata dawa kwani deni hilo likilipwa changamoto ya ukosefu wa dawa kwenye vituo na zahanati utapungua.
Mwenyekiti huyo aliwakumbusha madiwani kufatilia na kusimamia vyema miradi iliyopo kwenye kata zao lakini pia aliitaka halmashauri kuhakikisha inawajulisha madiwani pindi wanapopeleka miradi kwenye kata zao na kuahidi kufatilia utekelezaji wa miradi yote kwa kipindi cha 2018 hadi 2021.
Awali Januari 25,2021 Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira akitembela kituo cha afya Nyangoto alibaini changamoto mbalimbali zikiwemo za uhaba wa dawa.
Mbunge huyo alimwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa kuhakikisha sh.Mil 185 ambalo ni deni la MSD linalipwa pamoja na kufanya mabadiliko makubwa ya usimamizi wa huduma ya afya katika halmashauri hiyo.
Alisema kuwa mabadiliko hayo yakifanyika yatasaidia kuondoa malalamiko mengi ya wananchi ambao wengi wao wanapata huduma kwenye vituo na zahanati za serikali.
Waitara alisema wananchi wasipopata huduma nzuri,huisema vibaya serikali na chama cha Mapinduzi (CCM) jambo ambalo halimpendezi kwakuwa kazi yake ni kuhakikisha anatatua kero zinazowakabili wananchi wa jimbo lake.