Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Bwana Jaffari Matundu (katikati) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akizungumza kuhusu utendaji wa benki hiyo katika kipindi cha mwaka 2020. Wengine ni Mkuu wa Idara ya Mikopo wa benki hiyo Bi Zainab Nungu , (Kushoto) na Afisa Mkuu Idara ya Fedha Bwana Shani Kinswaga.
NA MWANDISHI WETU
Benki ya Exim (Group) imetangaza kupata faida ya jumla ya TZS 25.3 Bilioni (kabla ya kodi) kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na hasara ya kiasi cha TZS 8.4 Bilioni iliyopata kwa mwaka uliopita, hatua inayoakisi ukuaji wa asilimia 402% wa Mwaka hadi Mwaka (YoY).
Mafanikio hayo yanayotajwa kuwa yametokana na ufanisi wa kiutendaji licha ya changamoto za kiuchumi kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ulioathiri ukuaji wa uchumi katika baadhi ya sekta muhimu nchini mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo jijini Dar es Salaam leo imebainisha kuwa benki hiyo imetekeleza kwa ufanisi mkubwa mkakati wa kushirikiana na sekta zinazofanya vizuri sambamba na kuongeza umakini zaidi katika matumizi yake ili kuongeza tija zaidi katika utendaji.
“Katika kipindi hicho benki ilikuwa bega kwa bega na sekta zilizoathiriwa wakati wa janga hilo na kwa kweli tulishirikiana kikamilifu na wateja wetu kuhakikisha kwamba si tu tunawapatia fedha bali pia tunawajengea uwezo wa kuweza kufanya shughuli zao katika kipindi hicho kigumu.’’ Alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa wa benki hiyo Bw. Jaffari Matundu.
Kwa mujibu wa Bw Matundu, hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2020, benki hiyo ilikuwa imetoa msamaha wa zaidi ya TZS bilioni 290 kwa njia ya likizo ya malipo na upanuzi wa vipindi vya ulipaji wa mikopo ili kusaidia wateja wa benki hiyo ambao biashara zao ziliathirika zaidi na athari za kiuchumi za Covid-19.
"Tunayo furaha kuripoti matokeo mazuri kwa mwaka wa fedha 2020. Tumefanikiwa kurejesha asilimia 9.0 ya faida kwenye mfuko wa wanahisa ikilinganishwa na marejesho hasi ya asilimia 9.2 mnamo 2019" alisema Bwana Matundu katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Nchini Tanzania, benki hiyo ilirekodi mafanikio makubwa kwa kupata faida (kabla ya kodi) ya Shilingi Bilioni 18.8 kutoka kwenye hasara ya TZS Bilioni 14.5 (kabla ya kodi) ya mwaka uliopita.
"Mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa mali kufuatia usafishaji uliofanywa katika kipindi hicho cha mwaka uliopita hatua Iliyosababisha kupungua kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 22.3 ya mwaka 2019 hadi kufikia asilimia 7.4 kwaka 2020.''
"Matawi yetu ya nchini Djibouti na Comoro pia yalirekodi faida ya TZS Bilioni 4.9 na Bilioni 5.7 (kabla ya kodi) licha ya athari ya COVID-19.
“Jumla ya Mali zetu imebaki kuwa TZS 1.9 Trilioni. Amana za wateja zimeongezeka kwa 4.4% wakati wa robo ya mwaka na kufikia Shilingi Trilioni 1.38. Shughuli zetu nchini Tanzania, Comoro na Uganda zote zimerekodi ukuaji wa ajabu katika amana za wateja wakati wa robo ya mwisho wa mwaka”aliongeza
Alisema mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yanachochewa na kauli mbiu ya benki hiyo "Exim Kazini Leo kwa ajili ya Kesho' ambayo imekuwa ikiisukuma benki hiyo kubuni huduma mpya zinazoendana na mahitaji ya wateja wake.