Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DAKTARI BINGWA AONDOA GUNDI KALI KWENYE NGOZI YA KICHWA CHA MREMBO ALIYEPAKA AKIDHANI MAFUTA YA NYWELE



Mrembo baada ya gundi kuondolewa kwenye kichwa chake
Dkt Michael Obeng 

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile,Michael Obeng, Mmarekani mwenye asili ya Ghana,amefanikiwa kuondoa gundi iliyokuwa imegandishwa kwenye ngozi ya kichwa cha mwanamke mmoja aliyeonesha kichwa chake kwenye video mtandaoni.

Mwanamke huyo alijipaka gundi hiyo bila kujua akidhani ni mafuta ya kurembesha nywele zake, kwa mujibu wa video za TMZ.

Dkt. Michael Obeng alichukua saa nne kuondoa gundi hiyo kutoka kwa kichwa cha Tessica Brown, tovuti hiyo imeandika.

Daktari huyo bingwa aliyesomea chuo kikuu cha Havard, ambaye sasa hivi anaendesha shughuli zake katika eneo la Beverly Hills alijitolea kufanya upasuaji huo ambao ungegharimu dola 12,500 bila malipo baada ya kusikia masaibu yaliyompata Bi. Brown ambaye alishirikisha wengine yaliyompata kupitia video ya TikTok wiki iliyopita.

Mwanamke huyo alikuwa ametumia gundi inayotumiwa kugandisha vigae, sakafu za mbao na mapambo ya nyumbani na kulazimika kukata nywele ambazo alikuwa amebandika kwasababu zilikuwa zinavuta ngozi yake sana.

Social embed from youtube

Baada ya kupata matibabu, Bi. Brown aliyejawa na hisia alionekana akipitisha vidole vyake kwenye nywele zake.

Dkt. Obeng, ambaye ana historia ya kufanya kemia, ameelezea TMZ kwamba alitumia kemikali mbalimbali kulainisha kiungo cha msingi (polyurethane,) kwenye gundi hiyo aina ya Gorilla Glue.

Alisema alifanya utafiti huo na kufanikiwa kutengeneza mchanganyiko wa kemikali kuondoa gundi hiyo iliyojumuisha aloe vera, mafuta ya mzaituni na nyinginezo.

Baada ya kumaliza kutengeneza mchanganyiko huo, kwanza alijaribu katika nywele zilizokuwa zimegandishwa kwa aina hiyo ya gundi ili kuhakikisha kwamba itafanya kazi.

“Ana bahati kwasababu hakupata majeraha makubwa katika ngozi yake ya kichwa. Aina hii ya gundi huwa sio mchezo,” alisema, na kuongeza kuwa gundi hiyo ilifanya nywele zake na kuzigandisha kama kijiti.

Alitoa wito kwa watu kuwa makini zaidi na kusoma vichupa vya kemikali mbalimbali wanavyonunua kabla ya kuanza kutumia bidhaa hizo.

Dkt. Obeng amebobea katika upasuaji wa kubadilisha maumbile na kulingana na tovuti hiyo, yeye ndio mwanzilishi wa shirika ambalo hufanya upasuaji wa bure katika mataifa yanayoendelea kukua na pia hutoa mafunzo kwa madaktari wa eneo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com