Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema bendera za chama hicho katika ofisi zake zote zitapepea nusu mlingoti kama ishara ya kuomboleza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kabla ya kujiunga ACT-Wazalendo na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif alikuwa katibu mkuu wa CUF anayetajwa kuwa mzizi wa kuimarika kwa CUF Zanzibar na Tanzania Bara.
Maalim Seif amefariki dunia leo saa 5 asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi
Profesa Lipumba amesema atamkumbuka Maalim Seif kwa namna alivyoshiriki kuijenga CUF.
“Ni msiba mkubwa kwa Taifa na alikuwa mkongwe katika siasa, ni muasisi wa chama (CUF) hivyo bendera zetu zitapepea nusu mlingoti kukumbuka mchango wake katika chama.”
“Aliwahi kuwa katibu mkuu tangu mwaka 1999 hadi 2019 na kabla alikuwa na makamu mwenyekiti wa chama,” amesema Profesa Lipumba
Amesema yeye na Maalim Seif wamejuana tangu mwaka 1973 wakiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) wakihudumu katika vitengo na nafasi tofauti.