Rais Dk John Magufuli ametuma salamu za pole kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, wanachama wa ACT- Wazalendo pamoja na familia ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia leo Jumatano Februari 17, 2021.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, kiongozi mkuu huyo wa nchi ameandika, “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi amina.”
Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi, alisema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.
''Majira ya saa tano na dakika 26 asubuhi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia, Maalim amefariki wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa tangu tarehe 9 mwezi Februari mwaka huu'', amesema Rais Hussein Mwinyi.
Rais Mwinyi amesema taifa limepoteza kiongozi mzalendo na shupavu na ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti.
Rais Mwinyi amesema taarifa zaidi kuhusu msiba na maziko yake zitaendelea kutolewa na serikali, kwa ushirikiano wa karibu na familia na Chama cha ACT- Wazalendo.
Social Plugin