Baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992. Maalim Seif alibaki kuwa mpinzani nambari moja kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndani ya visiwa vya Zanzibar.
Ni tofauti na upande wa Tanzania bara ambako nguvu za kiongozi wa upinzani daima zinabadilika.
Tangu akiwa na chama chake cha Chama cha Wananchi (CUF) hadi akiwa na ACT Wazalendo. Nguvu zake kisiasa zilikuwa kubwa sana. Ni nguvu zilizokuwa na uwezo wa kuamua kati ya utulivu au vurugu ndani visiwa vya wakaazi milioni moja na nusu.
Aliheshimika kwa misimamo yake na kutotetereka.
Kwa sababu ya uungwaji mkono mkubwa aliokuwa nao, baadhi ya wadadisi wa siasa waliamini Maalim Seif ndiyo chama na chama ndiyo Maalim.
Ukweli wa hilo ulidhihirika baada ya kuhama CUF na kwenda ACT Wazalendo.
Kwanini Maalim alirudi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa?
Kilikuwa ni kitendawili cha kisiasa pale Maalim Seif na chama chake cha ACT Wazalendo walipoamua kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya uchaguzi wa Oktoba 2020.
Swali kubwa lililoulizwa, kwanini kaingia katika serikali ambayo aligoma kutambua ushindi wa Rais wake?
Sababu ya Maalim Seif na (CUF), kususia uchaguzi wa marudio wa 2015, ni madai ya wizi na kuporwa ushindi. Pia madai yakawa ni hayo hayo katika uchaguzi uliopita, ambao ulishuhudia upinzani bara na visiwani ukipoteza viti vingi mno.
Nimemuuliza mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Khalid Gwiji, akiwa Toronto, Canada; kipi kilimrudisha Maalim na chama chake katika serikali ya umoja wa kitaifa licha ya madai ya kutokea wizi wa kura?
"Ni uzalendo wake kwa Zanzibar. Waliweka mbele maslahi ya nchi katika nyanja zote, ukianzia siasa na uchumi. Na walielewa kutoshiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa kungeendeleza mgawanyiko na matatizo kwa Zanzibar."
31 Julai, 2010 Wazanzibari walishuka vituoni kupiga kura ya 'Ndio au Hapana' kuamua ikiwa wanataka muundo wa kiutawala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ama la. Hatimaye, zaidi ya asilimia 60 walipiga kura ya ndio.
Uchaguzi wa 2010 serikali hiyo ikaanza kufanya kazi chini ya Urais wa Dkt. Ali Mohammed Shein, wa Chama cha Mapinduzi, (CCM) na Makamu wa kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, wa Chama cha Wananchi (CUF).
Wakati serikali hiyo ikiwepo madarakani 2010 hadi 2015, Zanzibar ilishuhudia ahueni kubwa kuanzia katika uchaguzi wa 2010. Zile ripoti za makundi ya watu wanaovamia na kupiga watu wakati wa uchaguzi hazikuwepo.
Hata matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa wafuasi wa vyama vikuu shindani, CUF na CCM walisherehekea ushindi kwa pamoja katika mitaa ya Zanzibar.
Huku Maalim akieleza katika hotuba yake ya kukubali kushindwa, kwamba ushindi huo ulikuwa ni wa Wazanzibari wote.
Mwinyi na Maalim
Siku mia za utawala wa Dkt. Hussein Mwinyi na Maalim akiwa makamo wa kwanza wa Rais, zilitoa mwanga wa matumaini juu ya mwelekeo mpya wa kiuongozi na kisiasa ndani ya Zanzibar. Kulidhihirika mshikamano na maridhiano.
"Kwanini uongozi wa Mwinyi na Maalim ulionekana kuendana?'
Nimemuuliza tena Khalid Gwiji.
"Maalim na chama chake walimuona Dkt. Mwinyi yuko tofauti, hakuwa mtu wa siasa za majungu wakati wa kampeni. Hata alipoingia madarakani walimpa muda na wakamuona ni kiongozi tofauti, alikuwa anasisitiza umoja na ushirikiano wa Wazanzibari."
Zanzibar kuyapata thamani mazao ya bahari
"Uongozi wake ulitoa matumaini kwamba ni kweli anataka mageuzi ndani ya Zanzibar. Aina yake ya uongozi ilimshawishi pakubwa Maalim na ACT Wazalendo kukubali kuwa sehemu ya serikali."
Wahenga husema, "chema hakidumu". Ndoa ya Maalim Seif na Dkt. Hussein Mwinyi ilikuwa tofauti na ile ya Maalim na Dkt. Ali Mohammed Shein. Ingawa zote ni ndoa za kisiasa lakini zilikuja na ladha tofauti.
Ndoa iliyoonekana kuja na ladha nzuri kwa Wazanzibari, yaani kati ya Maalim na Mwinyi ndio ambayo haikudumu muda mrefu. Mkongwe katika siasa za visiwani anaondoka wakati zimepita siku mia tu tangu Mwinyi aingie madarakani.
Kauli za Maalim mwenyewe zilionesha kuridhishwa na aina ya uongozi wa Dkt. Mwinyi. Akieleza kwamba anafarijika na utawala huu. Akitolea mfano kwamba ushauri wanaotoa unasikilizwa na kufanyiwa kazi, hilo ni tofauti na wakati wa Dkt. Shein.
Kwa maneno mafupi, Mwinyi na Seif walikuwa ni tumaini jipya kwa Wazanzibari wote. Siasa hazitoi uhakika ikiwa mambo yangeenda kama yalivyoanza, bali lenye uhakika ni kwamba walianza vyema uongozi wao.
Kaiacha Zanzibar katika sura gani?
Ikiwa Maalim angeaga dunia mwaka 2016, 2017, 2018 ama 2019, angekuwa ameondoka huku kaiwacha Zanzibar katika mchafukoge mkubwa wa kisiasa na kijamii.
Je, kwa sasa anaiacha Zanzibar katika sura ipi?
Swali hilo nimemuuliza mwandishi wa habari na mchambuzi wa siasa, Abdulfatah Mussa, akiwa katika jiji la Tehran nchini Iran.
"Alikuwa na nembo tatu, alipigania maendeleo ya Zanzibar, umoja na maridhiano ya Wazanzibari na tatu alipigania Zanzibar kuwa na haki sawa katika Muungano. Ameondoka na kaiwacha nchi katika msingi mzuri wa maridhiano na umoja wa Wazanzibari."
"Na kwa kauli yake mwenyewe alisema amefarijika pakubwa na serikali ya Dtk, Mwinyi, inapinga ufisadi, ubaguzi na ina kiu ya maendeleo ya Zanzibar. Kwahiyo anaondoka kukiwa na mwanga wa matumaini kwa nembo zake mbili. Limebaki swala la usawa wa Zanzibar katika Muungano."
Waswahili husema, 'kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi.' Kuondoka kwa Maalim Seif hakupaswi kuwa mwisho wa siasa za maelewano, ambazo alishiriki kuziasisi upya akiwa na Rais Mwinyi baada ya kuvunjika 2015.
Zanzibar daima imekuwa na siasa ngumu, zenye kuwafanya watu kuchukiana na hata wakati mwingine kupoteza maisha. Mshikamano aliouwacha utaendelea kuwa muhimu mno kwa mustakbali wa Zanzibar njema huko usoni.
Utulivu uliopo sasa haupaswi kuwa wa miaka mitano. Wala haupaswi kuondoka kwa sababu ya kifo cha Maalim. Rais Dkt. Mwinyi atakuwa na kazi ya kuyaendeleza yale walioanza kuyasimika na makamo wake wa kwanza wa Rais.
Via BBC Swahili