Makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nchini Kenya wamemkamata mwanaume aitwaye John Christon Shipiti mwenye umri wa miaka 52 kwa madai ya kumuua mwanafunzi wa Darasa la 8 kwa kumharibu bintiye.
Ripoti zilionyesha kwamba mtuhumiwa, John Christon Shipiti alimshambulia mwanafunzi huyo wa miaka 17 kutoka shule ya msingi ya Chemego kwa tuhuma za kumnyemelea bintiye mwenye miaka 13.
Kulingana na ripoti ya DCI, marehemu alipata majeraha mabaya na aliripotiwa kufariki dunia tayari alipofikishwa katika hospitali ya Vihiga kutibiwa.
"Mwathiriwa aliachwa na majeraha mabaya miguuni, katika paji la uso, mashavuni na mdomoni baada ya kupokezwa kichapo. Kisa hicho hata hivyo kilifichwa hadi jana," ripoti ya DCI ilisema.
Polisi walisema kuwa mshukiwa atasalia korokoroni akisubiri kufikishwa mahakamani.
Katika kisa kingine cha kutisha, baba wa binti wa umri wa miaka 18 alikamatwa na kuzuiliwa kwa madai ya kumdunga kisu mpenzi wa msichana wake.
Ripoti ilisema kwamba mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 alimdunga kisu mvulana huyo baada ya kumfumania bomani mwake akiwa na bintiye.
Mshukiwa angali anazuiliwa katika kituo cha polisi huku polisi wakiendelea na uchuguzi wao.
Visa hivyo vinajiri wakati idara ya DCI imetangaza kukaza kamba katika kukabili visa vya uhalifu nchini.
DCI ilizindua nambari ya simu bila malipo ya 0800722203, ambayo umma unaweza kutumia kuripoti uhalifu kwa idara hiyo bila kutambulika.
Hatua hiyo inakusudiwa kuhakikisha kuwa visa vya uhalifu vinawafikia polisi haraka iwezekanavyo.
Chanzo -Tuko News