Baadhi ya mifugo wanaopatikana katika kituo cha utafiti wa Mifugo cha TALIRI Mpwawa mkoani Dodoma.
Na Faustine Gimu Galafoni, Dodoma.
Halmashauri zote nchini zimetakiwa ziwe na shamba darasa ya malisho ya mifugo ili kupunguza migogoro ya ardhi kutokana na wafugaji kuvamia maeneo ya wakulima kwa lengo la kutafuta malisho.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara ya Utafiti Wizara ya Mifugo Dk. Anjelo Mwilawa wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha utafiti wa mifugo [TALIRI] Mpwapwa ambapo alibainisha kuwa licha ya nchi ya Tanzania kuwa na wingi wa mifugo lakini maeneo ya malisho ni ya tangu miaka ya nyuma .
“Malisho haya ya nyasi yanatuletea virutubisho vya wanga kwenye vyakula vya wanyama ,katika maeneo haya ya nyanda kame tuhimize wafugaji wetu wastawishe malisho ambayo yatakuwa chanzo cha chakula bora kwa mifugo yao ,wizara yetu imehimiza halmashauri kuwa na mashamba darasa ya malisho ili wafugaji waweze kupata mbegu bora na kuepika migogoro ya ardhi”,alisema.
Msimamizi wa shamba Darasa la malisho ya mifugo Mpwapwa Erick Kimaro amesema shamba hilo limekuwa na tija kubwa kwa malisho ya mifugo.
“Tumepanda nyasi hizi ambazo ni muhimu sana kwa malisho ya mifugo na eneo lina ukubwa wa hekta 120 sawa na wastani wa ekari 240 na tumekuwa tukipokea wafugaji kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya Kiteto”,amesema.
Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya utafiti mifugo nchini [TALIRI] DK. Jonas Kizima amezungumzia majukumu ya taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kutatua changamoto za wafugaji na kufanya tafiti mbalimbali.
“Taasisi ya utafiti wa mifugo Tanzania [TALIRI]ipo chini ya wizara ya mifugo na Uvuvi na imeundwa kwa sheria Na.4 2012 ,na inayo majukumu ambayo ni kufanya tafiti na kutatua changamoto za wafugaji na inaundwa na kanda saba kote nchini ”,amesema.
Kaimu Meneja wa Idara ya Utafiti wa Mifugo TALIRI kituo cha Mpwapwa Deogratius Massawe ameelezea historia ya josho la Nunge Mpwapwa ni tangu mwaka 1905 ambapo wakoloni waliona eneo hilo ni muhimu kwa sababu ya ufugaji.
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania [TALIRI ]tayari imefanya utafiti wa malisho ya mifugo katika kituo chake cha Mpwapwa na wizara ya mifugo na uvuvi imeshauri ni vyema utafiti ufanyike kwa kutumia halmashauri ili ku punguza migogoro ya ardhi ambapo Kituo cha Utafiti wa Mifugo Mpwapwa ni kituo cha kwanza kuanzishwa nchini chini ya utawala wa wakoloni wa Kijerumani 1905 na hadi kufikia sasa ni zaidi ya miaka 115.
Social Plugin