Mstahiki Meya, David Nkulila akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Shinyanga leo Februari 12, 2021 baada ya kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Sh Bilioni 31.4 kwa mwaka 2021/2022. Nkulila ushirikiano baina ya watendaji wa halmashauri hiyo katika kutekeleza maazimio ya baraza la madiwani ili kuifikia azma ya kuwa jiji na kupandisha uchumi wa mji wa Shinyanga. Amesema wanaobeza wazo la Madiwani kuifanya Jiji, Manispaa ya Shinyanga wataumbuka.
Mstahiki Meya, David Nkulila (kulia) akisisitiza jambo kwa madiwani wa manispaa ya Shinyanga wakati wa kikao cha kupitisha mapendekezo ya bajeti. Kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Geofrey Mwangulumbi
Kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Shinyanga kikiendelea
Kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Shinyanga kikiendelea
***
Na Damian Masyenene, Shinyanga
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga kwa kauli moja wamepitisha mapendekezo ya mpango wa bajeti wa Sh. Bilioni 31.4 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Mapendekezo hayo yamepitishwa leo Februari 12, 2020 katika siku ya pili ya kikao cha baraza la madiwani la manispaa hiyo katika ukumbi wa halmashauri mjini Shinyanga, ambapo mapendekezo hayo yameainisha kile ambacho halmashauri hiyo itakusanya na kutumia kwa mwaka 2021/2022.
Akitangaza maazimio ya baraza hilo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila ameeleza kuwa bajeti hiyo ya Shilingi Bilioni 31.4 itatokana na makusanyo ya vyanzo vya ndani Sh Bilioni 4, ruzuku ya mishahara Sh Bilioni 22.7, ruzuku kutoka Serikalini Sh Bilioni 1.5, ruzuku kutoka kwa wadau wa maendeleo na wahisani Sh Bilioni 1.9 na zingine Sh Bilioni 1.1.
Akisisitiza juu ya azma ya kuifanya manispaa hiyo kuwa jiji na kuhakikisha kuwa kile kilichoazimiwa na madiwani ndicho kitakachotekelezwa, Mstahiki Meya huyo ameutaka uongozi wa manispaa hiyo chini ya Mkurugenzi Geofrey Mwangulumbi kuhakikisha wanajenga nidhamu ya bajeti na kuheshimu maamuzi ya madiwani kama ambavyo huwa wanaheshimu maagizo ya viongozi wakubwa wakiwemo mawaziri.
“Niombe sana mkurugenzi, huu mtindo wa kuheshimu maagizo kwa kuangalia yametoka wapi tuuache na uheshimu kile kilichoamuliwa na madiwani sawa na mnavyoheshimu maagizo ya wakubwa….Tuombe mjaribu kuziba mwanya huu wa kukiuka kilichoamuliwa, ili tuwaumbue wote waliotubeza kuhusu wazo letu la kuifanya Shinyanga kuwa jiji.
“Mimi siko tayari kuaibishwa na Rais, kwahiyo naomba ushirikiano wenu maazimio ya baraza yaheshimiwe, kuzingatiwa na utekelezaji ufanyike, hatutaki mambo yale ya kila siku kwamba tuwape muda na msisubiri mpaka mawaziri waje hapa kuwashurutisha,” amesisitiza Nkulila.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Kaimu Mkurugenzi, Dorice Dario, amesema kuwa halmashauri itafanya kazi kwa ukaribu na madiwani na kwamba mchakato huo utakwenda kadri walivyopanga na hatimaye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuipitisha bajeti yao ya Sh Bilioni 31.4.
Kabla ya kujadili mapendekezo hayo ya bajeti, madiwano hao walipokea taarifa ya mrejesho wa ombi la kumilikishwa eneo la Tanganyika Packers kuwa eneo la uwekezaji wa viwanda lenye ukubwa wa ekari 1,058 lililopo katika kijiji cha Ihapa kata ya Old Shinyanga, ambalo kwa sasa linatumika kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mtakwimu wa Manispaa ya Shinyanga, Fidelis Kabuje ameeleza kuwa eneo hilo lilitengwa kwa mara ya kwanza Septemba 9, 1950 kwa ekari 80 kutumika kujenga kiwanda cha nyama ambacho hakifanyi kazi hadi sasa na ekari zingine 1,058 kwa ajili ya malisho ya mifugo na kwa sasa halina shughuli endelevu.
Ambapo, tayari ramani imechorwa na kupatikana viwanja 426 na mkakati ni kuwagawia viwanja bure wananchi na wawekezaji ambapo serikali itanufaika kwenye kodi za hati ya viwanja, ambapo kupitia ramani hiyo eneo hilo litakuwa na kituo cha mabasi, soko na viwanja vya makazi 100.
Wakichangia hoja juu ya taarifa hiyo, madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga waliunga mkono ombi la kulimilikisha kwa halmashauri hiyo eneo hilo ambalo lipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Diwani wa Kata ya OId Shinyanga lilipo eneo hilo, Enock Lyeta (CCM), amedai kuwa eneo hilo limekuwa tatizo kwa wananchi kwani lilikuwa halileti tija kwa maendeleo ya manispaa hiyo kwa kuwa limekaa muda mrefu bila kuendelezwa, hivyo kumilikishwa kwa manispaa hiyo kutasaidia kuupanua mji wa Shinyanga na kuifikia azma ya kuwa jiji.
Naye Diwani wa Kata ya Kambarage, Hassan Mwendapole (CCM), ameeleza kuwa kiwanda kilichojengwa katika eneo hilo hakijawahi kufanya kazi na wawekezaji walitumia eneo hilo kwa maslahi yao kupata mikopo, ambapo ameiomba wizara ya viwanda na biashara kuwaunga mkono kwani lengo ni kuupanua mji na kuliendeleza eneo hilo.
Kwa Upande wake, Mstsahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amesema kuwa hoja hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack mbele ya Rais Dk. John Magufuli katika ziara yake mjini Kahama kwa niaba ya Wana Shinyanga, hivyo wanampongeza.
“Mmetuagiza twende Dodoma tukashauriane na watu wa wizara, niwahakikishie madiwani mimi kama mwakilishi wenu nitalifikisha hili na mbunge ametuhakikishia kwamba ataungana nasi. Naamini kwa hoja zetu tutakuwa na sababu za kumshawishi waziri kwasababu lengo ni kuupandisha uchumi, kuongeza uwekezaji na kuuendeleza mji wetu,” ameeleza.
Via Shinyanga Press Club blog
Social Plugin