Mwenyekiti wa soko kuu Alex Stephen akizungumza kwa niaba ya wananchi
Naibu Waziri wa Mazingira Mwita Waitara akikagua dampo la kisasa la manispaa linalijengwa maeneo ya Nhelegani manipaa ya Shinyanga
Naibu Waziri wa Mazingira Mwita Waitara akizungumza na wakuu wa idara wa mkoa wa Shinyanga na wa manispaa baada ya kumsomea taarifa ya mkoa wa Shinyanga.
Suzy Luhende Shinyanga.
Wafanyabiashara wa soko kuu Manispaa ya Shinyanga wametoa kilio chao mbele ya Naibu Waziri wa Mazingira Mwita Waitara wakidai kuwa hawafanyi biashara kwa sababu ya kuondolewa magari na kupelekwa stendi ya zamani yaliyokuwa yakileta wateja kutoka wilayani Kishapu na sehemu zingine na kwamba soko hilo ni chafu halina mitaro ya kupitisha maji.
Pia wamelalamika kuwa dampo la taka limekuwa likijaa lakini taka hizo hazitolewi kwa wakati na wanapotoa taarifa katika manispaa wanajibiwa kuwa gari la kuzoa taka ni bovu, hivyo uchafu huo kulazimika kuendelea kujaa na kumwagikia nje ya dampo kwa muda mrefu bila kuzolewa.
Malalamiko hayo wameyatoa jana kwa Naibu Waziri wa Mazingira Mwita Waitara alipokuwa kwenye ziara ya siku moja ya kukagua madampo, masoko na kuangalia mfumo wa madampo kama ujenzi wake unazingatiwa na usafi unafanyika ili kuepukana na magonjwa ya milipuko yanayosababishwa na uchafu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi mwenyekiti wa soko hilo Alex Stephen alisema kuna changamoto kubwa katika soko hilo ambapo taka haziondolewi kwa wakati licha ya kwamba wanachangia kila mmoja kwa mwezi 1500 lakini taka haziondolewi hivyo kumuomba awasaidie kwa sababu wanaona hakuna wa kuwajali.
lsaya Athuman na Rajabu Issa mfanyabiashara wa soko hilo amesema kwa sasa wanaishi maisha magumu kwa sababu hawana wateja waliokuwa wakiwategemea kwani wote wanashushuwa katika stendi ya zamani ambayo inapakana na soko la Nguzo nane, hivyo wateja wakishuka wanaenda pale kwa vile ni karibu wao wanaachwa.
Kwa upande wake Mrugenzi wa Manispaa hiyo Geofrey Mwangulumbi amesema kuwa taka zinaingiliana na taka za watu wanaoishi karibu na soko hilo na si wote ambao wanachangia hiyo fedha ndiyo maana wakati mwingine uzoaji unachelewa kutokana na kijiko cha kuzolea kinakuwa kwenye matengenezo.
"Pia kuhusianana magari tuna mpango mzuri wa kuleta magari ambayo yatakuwa daladala za hapa mjini sio baiskeli tena. Magari hayo yatakuwa yanapaki hapa ndiyo maana hapo mmeona miundo mbinu ya kupumzikia wateja imetengenezwa, hivyo Jumanne nitakuwa na kikao nanyi tuje tuzungumze hapa naomba mhudhurie wote tutaelewana tu",alisema Mwangulumbi.
Walimuomba Waitara awasaidie kwa sababu shida wanazopata ni kubwa kwani wengine wana mikopo, hawana fedha ya kurejesha kwa sababu ya kukosa wateja, wanadaiwa na wengine wanafilisiwa.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Mazingira Mwita Waitara aliwataka wafanyabiashara hao watulie kwani serikali inashughulikia malalamiko yao.
Lakini pia aliwataka kuacha kutumia mifuko ya plastiki hata ile ya kuwekea maji kwa sababu ndio inayosababisha kuongezeka kwa taka, waendelee kutumia mifuko iliyopitishwa na serikali.
Aidha aliwataka waendelee kuchangia fedha kwa ajili ya kuzoa taka shilingi 1500 ili zisiendelee kujaa na kuwaahidi kuwa serikali ipo nao bega kwa bega itawasaidia na watafanya biashara kama kawaida.
Pia Waitara amekagua Dampo kubwa la kisasa linalojengwa katika maeneo ya Nhelegani manispaa ya Shinyanga ambalo litagharimu jumla ya Sh Milioni 200 ambalo litakuwa linatumika kutupa taka zote za manispaa na zitachujwa na maji taka kufanyia shughuli zingine za maendeleo mfano kufugia samaki au kutumika kama mbolea kwa ajili ya wakulima.