Mamlaka ya
Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) imetangaza kusitisha utoaji wa leseni za Maudhui
Mtandaoni kwa muda kuanzia Januari 28,2021 hadi Juni 30,2021.
Akizungumza
leo Jumatatu Februari 1,2021 kwenye Usiku wa Waandishi wa Habari na Wadau wa
Habari Kanda ya Ziwa katika ukumbi wa Gold Crest Hotel Jijini Mwanza, Mkuu wa
TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo amesema hatua ya kusitisha utoaji leseni
kwa Blogs na Online Tv inatokana na kuendelea kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa
matumizi sahihi ya mtandao.
“Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuanzia tarehe 28 Januari, 2021 imesitisha utoaji leseni za
maudhui mtandaoni kwa muda hadi tarehe 30 Juni 2021 ili kutoa fursa kwa TCRA
kufanya tathmini na kuja na hatua muhimu za kurekebisha dosari nyingi
zilizojitokeza”,amesema Mhandisi Mihayo.
Mhandisi
Mihayo pia amewataka watoa huduma wa sekta ya utangazaji kutekeleza matakwa ya
kanuni ya uendeshaji ikiwemo kuwalipa mishahara watumishi wao.
Aidha
amewasihi waandishi wa habari kupendana na kushirikiana na kuhakikisha
wanajiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya Diploma ili kukidhi
vigezo vinavyotakiwa.
Social Plugin