Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Agnes Ginethon akitoa elimu ya ukatili kwa wajumbe wa Kamati ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kata ya Mwamala
Na Suzy Luhende - Shinyanga
Wanaume wa kata ya Mwamala katika halmashauri ya Shinyanga wametakiwa kuzungumza na watoto wao wa kike ili kuondokana na ukatili wa ndoa za utotoni, mimba za utotoni na magonjwa ya kuambukizana kama vile Virusi vya Ukimwi.
Hayo yamebainishwa na kamati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika kata ya Mwamala halmashauri ya Shinyanga vijijini ambapo walisema wanaume ni vizuri wazungumze na watoto wa kike ili kuondokana na ukatili huo.
Walisema akina baba wengi hawazungumzi na watoto wao wa kike wamekuwa wakiwaachia wanawake pekee hali ambayo imekuwa ikisababisha watoto wa kike kuambukizwa magonjwa na watoto wa kiume ambao wamezaliwa na maambukizi, kupata mimba za utotoni, na kusababisha ndoa za utotoni.
Akitoa elimu kwa wanakamati hao, Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Agnes Ginethon alisema ili kuweza kutokomeza ukatili kwa watoto wa kike kina baba wanatakiwa wabadilike wazungumze na watoto wao wa kike, kwani wamekuwa wakiogopa kuzungumza na watoto hao kutokana na mila na desturi ya kwamba mtoto wa kike yeye anazungumza na mama tu na mtoto wa kiume ndiye anazungumza na baba.
"Ndugu zangu hali ya sasa imebadilika tunanatakiwa kuachana na mila na desturi tuzungumze na watoto wetu wote tusibague, na nyinyi baba ndiyo chanzo kikubwa cha watoto kupata mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na kupata magonjwa ya kuambukizana kwa sababu hamzungumzi na watoto wenu mnaogopa kuzungumza nao huku mmewazaa nyinyi wenyewe", alisema Agnes.
"Mnatakiwa kuwaambia bila kuwaogopa kwa sababu nyakati hizi kuna watoto wenzao wamezaliwa wakiwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, msipowaambia kwamba acheni kuwazoea wanaume kuna madhara haya na haya watajikuta wanachezeana wao kwa wao na kuachiana magonjwa, hivyo tuzungumze nao ili kuwaepusha waweze kuwa na afya salama na kutimiza ndoto zao",aliongeza.
Shimba Mhoja ambaye ni mgambo kutoka ofisi ya kata Mwamala alisema kweli katika maeneo wanayoishi kina baba hawakai na kuzungumza na watoto wao wanawaachia mama zao wao wanazungumza na watoto wa kiume peke yao labda kwa vile wamepata elimu na wamefundishwa jinsi ya kuongea nao watabadilika.
"Sisi wanaume kweli tulikuwa tunajua watoto wa kike wanafundishwa na wanawake, lakini kwa sababu tumeelimishwa tutakuwa tunakaa nao na tutaenda kuzungumza na watoto wetu kuanzia leo na tutaenda kuwaelimisha wanaume wenzetu ili waweze kuelewa na waweze kuwa wanakaa na watoto wao na kuwaeleza madhara yatakayopatikana endapo watadanganywa na wanaume au na wanafunzi wenzao", alisema Mhoja.
Naye Ramadhan Dotto alisema mira na desturi bado inatumika ya wazazi wa kiume kuwaogopa watoto wao wa kike hivyo ndiyo maana ukatili wa kijinsia hauishi, lakini kwa sasa elimu itawafikia na watabadilika na kuweza kutokomeza ukatili wa kingono kwa watoto wa kike.
Kwa upande wake mtendaji wa kata ya Mwamala Suzan Kayange alisema ukatili bado upo katika kata hivyo ni vizuri elimu wanayopewa wakaifanyie kazi wawaelimishe na wengine ambao hawajaipata ili waache kufanya ukatili kwa watoto na kwa wanawake, na wanaume waache kuwafanyia ukatili watoto wao wa kike wazungumze nao kwa upana ili kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Ofisa Maendeleo ya Jamii kata ya Mwamala Sophia Philbert alisema wanaume wengi wa maeneo hayo kweli hawazungumzi na watoto wanawaachia wanawake peke yake na mwanamke ana kazi nyingi wakati mwingine anajisahau, hivyo ni vizuri wakasaidizana mme na mke kwa sababu malezi ni baba na mama.
Hata hivyo mashirika yasiyo ya kiserikali, halmashauri na Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga yenye mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto yamepewa fedha na Woman Fund Tanzania (WFT) kwa ajili ya kuelimisha jamii ya Shinyanga na kutokomeza ukatili wa kijinsia
Wajumbe wa kamati ya kutokomeza ukatili katika kata ya Mwamala wilaya ya Shinyanga wakipata elimu ya kuweza kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto
Social Plugin