Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akibofya kitufe kuzindua rasmi studio mpya za Channel Ten Plus TV, Radio Magic FM na Radio Classic FM katika jengo la Jitegemee mtaa wa Lumumba jijini Dar es salaam leo Alhamisi Februari 25, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli akifurahia wimbo wa “BABA” Wasanii Profesa Jay na Stamina wakati alipozindua rasmi studio za Channel Ten Plus TV katika jengo la Jitegemee mtaa wa Lumumba jijini Dar es salaam leo Alhamisi Februari 25, 2021.
PICHA NA IKULU
Habari na Herieth Makwetta - Mwananchi
Rais wa Tanzania, John Magufuli amekemea baadhi ya vyombo vya habari kushabikia na kueneza uzushi kuhusu vifo na kuvitaka kutumia haki na wajibu kuleta maendeleo kwa kutanguliza uzalendo na maslahi ya nchi.
Magufuli ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 25, 2020 katika uzinduzi wa studio ya televisheni ya Channel 10 na Magici FM na soko la Kisutu.
Amesema Serikali inavihitaji vyombo vya habari lakini ni vyema vikatanguliza uzalendo na haki ya anayeandikiwa.
“Pamekuwa na habari nyingi za uzushi zinatolewa kwamba fulani kafa, vigogo wafa, vigogo wapukutika mambo ya ajabu kabisa. Sisi Watanzania tunaombeana kufa, katika taarifa ambazo Taifa letu linachafuliwa unakuta watu wetu wanashangilia uzalendo umepungua.”
“Nawaomba wanahabari na Watanzania wote tutangulize uzalendo, yapo mataifa yanatokea mambo ya ajabu lakini huwezi kuona yameandikwa au kuwekwa kwenye mitandao, kila kitu hata kisichofaa kinaandikwa na hili si kwa waandishi wa habari pekee..., tutangulize maslahi na uzalendo wajenga nchi ni sisi na wabomoa nchi ni sisi,” amesema Rais Magufuli.
Alitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji kuwa wepesi kutoa taarifa na kwamba zipo wizara ambazo watendaji waandishi wakienda kuomba taarifa zinafichwa.
“Sisi tuwe wepesi kutoa taarifa mapema unakuta yamefanyika mambo mazuri katika wizara lakini hayatolewi. Tusiogope kukosolewa lazima tutoe ni haki kupata habari wahusika pande zote Serikali na vyombo vya habari viwe vyepesi kutoa taarifa za kweli bia kuweka chumvi huku wakizingatia uzalendo na ukweli,” amesema Rais Magufuli.
Awali Rais amesema sekta ya habari imeimarishwa ipasavyo hivyo ni haki na wajibu wa vyombo vya habari kuhakikisha vinathamini haki katika mambo ya habari , Serikali haichukii wanapoipatia changamoto.
“Mwaka 2015 tulikuwa na vituo vya redio 106 pekee nchi nzima lakini hadi leo tunavyo 193, televisheni zilikuwa 25 sasa tunazo 46, lakini mpaka sasa tumesajili redio 23 na televisheni 440 za mitandaoni kutoka sifuri mwaka 2015,” amesema na kuongeza kuwa leseni za majarida na magazeti zilizotolewa ni 247 na kuweka rekodi inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye vyombo vya habari vingi kuliko nchi yoyote Afrika.
CHANZO - MWANANCHI
Social Plugin