Serikali itawanyang'anya na haitowapa tena kazi ya kujenga miradi ya maji Wakandarasi wazembe walioshindwa kuitekeleza kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa tamko hilo Februari 25, 2021 wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa vijiji vya Buyagu, Kalangalala na Bototo Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Tamko hilo amelitoa kufuatia taarifa ya utekelezaji na hali halisi aliyoishuhudia ya mradi huo ambapo alieleza kusikitishwa na Mkandarasi mzawa aliyekuwa akiutekeleza.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) Sengerema, Mhandisi Cassian Wittike alisema ulikuwa ukitekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya D4N Construction Limited ya Wilayani Kahama ambaye alishindwa kuukamilisha kwa mujibu wa mkataba wake.
"Mradi huu ni miongoni mwa miradi tuliyorithi kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 2019 na haukuwa umekamilika kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi," alieleza Wittike mbele ya Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Aidha Mhandisi Wittike alisema kwamba mradi ulianza kutekelezwa tangu Desemba 2013 na ulipaswa kukamilika Juni, 2014 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7.
"Mkandarasi aliyepewa jukumu alishindwa na hivyo tuliuchukua na kuanza kutekelezwa na wataalam wa RUWASA Sengerema kuanzia mwaka 2019 na sasa hivi tupo kwenye majaribio na umeanza kutoa maji", alisema Mhandisi Wittike.
Kufuatia maelezo hayo na hali halisi ya mradi aliyoishuhudia, Naibu Waziri Mahundi alisisitiza kwamba Serikali haitamvumilia mkandarasi mzembe na badala yake atanyang'anywa mradi na atawekwa kwenye orodha ya wakandarasi ambao hawana sifa ya kukabidhiwa kutekeleza miradi ya maji kote nchini.
"Mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi inavyopasa atanyang'anywa mara moja na hatapewa tena kazi nyingine, hapo ajue amejifuta na ameingia rasmi kwenye orodha ya wakandarasi wasiokuwa na sifa wala uwezo wa kujenga miradi ya maji nchini," alisisitiza Mhandisi Mahundi.
Aliongeza kwamba hali ya uzembe wa baadhi ya wakandarasi hususani wazawa inamsikitisha Rais. Dkt. John Pombe Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba dhamira yake ya kuwainua haileti tija iliyokusudiwa.
"Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anafarijika kuona wakandarasi wazawa wanapata kazi ya kujenga miradi lakini bahati mbaya baadhi yao kwa kukosa uzalendo wanamuangusha kwa kushindwa kutekeleza vyema miradi wanayokabidhiwa," alisema Naibu Waziri Mahundi.
Mahundi alisisitiza kwamba Serikali imeonya wakandarasi wote wenye tabia ya kutumia fedha wanazolipwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji badala yake wanaipeleka kwenye masuala mengine yasiyohusiana na mradi.
"Wakandarasi mnapaswa kutambua fedha mnayolipwa ni kwa ajili ya kujenga miradi na siyo kufanyia matumizi mengine sasa bahati mbaya huwa fedha hii mnaipeleka kwenye matumizi tofauti na hapa ni lazima mshindwe kutekeleza miradi kwa ubora uliokusudiwa," alisisitiza Naibu Waziri wa Maji.
Social Plugin