Na Abby Nkungu, Itigi
HALMASHAURI ya Mji wa Itigi wilayani Manyoni mkoani hapa imetakiwa kuangalia kwa jicho la pekee suala la utoaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum kwa kuweka miundombinu yote muhimu shuleni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Wito huo ulitolewa mjini Itigi na baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022.
Mmoja wa madiwani hao Viti maalum ( Walemavu) tarafa ya Itigi, Mhe Amina Msita alisema licha ya Halmashauri hiyo kuwa na Shule ya msingi Mchanganyiko Mlowa ambayo ndio pekee inayochukua watoto wenye mahitaji maalum bado haina miundombinu rafiki kwa ajili ya kundi hilo.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kupitisha bajeti hii naomba kutoa angalizo juu ya Shule ya msingi mchanganyiko Mlowa yenye walemavu zaidi ya 40. Kuna haja ya kuongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu rafiki ya majengo kwa kundi hili" alisema na kuongeza;
Baadhi ya wanafunzi waliopo wanaishi kwa ndugu, jamaa au kwa walimu waliojitolea kuishi nao kutokana na ukweli kwamba wanatoka mbali, takriban kilomita 200 kutoka shule ilipo; hivyo kuna haja kwa shule hiyo kuongezewa madarasa, kujengewa mabweni, jiko na bwalo la chakula.
Alisema kuwa iwapo ujenzi wa miundombinu hiyo utafanyika na kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wenye mahitaji maalum sanjari na kupeleka walimu wa kutosha wenye ujuzi wa kufundisha elimu maalum, itasaidia kuondoa adha kwa wanafunzi wa kundi hilo.
Alisema lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanapata fursa ya kupata haki yao ya msingi ya kusoma bila kubaguliwa wala kuathiriwa na hali ya ulemavu wao katika kupata elimu.
Akiunga mkono hoja hiyo, Diwani wa Kata ya Itigi mjini, Ally Minja alisema kuwa suala la uwekezaji wa kudumu wa miundombinu ya majengo katika Shule mchanganyiko Mlowa haliepukiki kwa kuwa ndio shule pekee inayohudumia watoto wenye ulemavu katika halmashauri hiyo.
"Hii adha ya walemavu haiwahusu watoto wanaotoka mbali tu lakini hata wazazi walio karibu na shule hii bado wana kazi ya kumpeleka shule na kumrudisha nyumbani mwanafunzi mwenye ulemavu kwa kuwa hawezi kwenda shule na kurudi nyumbani peke yake hivyo kuna haja kubwa ya mabweni " alieleza
Alisema hivi sasa wazazi wengi wamehamasika kuwapeleka shule watoto wao wenye ulemavu baada ya kuona mabadiliko chanya kwa wale waliosoma na ndio maana hawawafichi tena majumbani hivyo ni jukumu ya halmashauri kuweka mazingira mazuri ya shule ili kutowakatisha tamaa.
Ofisa elimu ya msingi wa halmashauri hiyo, Doreen Lutahanamilwa alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapatiwa elimu, bila kujali hali yake ya maumbile; hivyo kila halmashauri imeagizwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa.
"Baada ya kufanya zoezi hili, tulibaini idadi kubwa ya watoto wenye mahitaji maalum wanaopaswa kwenda shule; hivyo tunakusudia kufungua Vituo vingine viwili vya Idondyandole na Mgandu. Aidha, tumebaini watoto hao wakiwekwa pamoja wanajisikia furaha".
Kikao hicho maalum cha baraza la madiwani kilipitisha jumla ya sh bilioni 22.75 ikiwa ni bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Social Plugin