BAO pekee la kiungo Muangola, Carlos Sténio Fernandes Guimaraes do Carmo, maarufu kama Carlinhos dakika ya 73 limetosha kuipa Yanga SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Carlinhos alifunga bao hilo dakika moja tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Ditram Nchimbi akimchambua kipa hodari wa Mtibwa, Abdultwalib Mshery baada ya kupokea krosi nzuri ya winga Mkongo, Tuisila Kisinda.
Awali ya hapo, Mtibwa Sugar walifanikiwa kuwabana vizuri Yanga tangu mwanzo wa mchezo na kuwaweka roho juu mashabiki wa Yanga ambao timu yao imetoka kutoa sare tatu mfukulizo katika Ligi Kuu.
Sare hizo ni 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City zote ugenini Sumbawanga na Mbeya na 3-3 nyumbani dhidi ya Kagera Sugar.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 49 baada ya kucheza mechi 21 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi saba zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, KMC imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, wakati Ihefu SC imeichapa 3-2 Mwadui Uwanja wa Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Ditram Nchimbi/Carlos Carlinhos dk72, Feisal Salum, Michael Sarpong/Abdulrazak Fiston dk65, Deus Kaseke/Farid Mussa dk65 Carlos Carlinhos na Tuisila Kisinda.Mtibwa Sugar; Abdultwalib Mshery, Hassan Kessy, Issa Rashid 'Baba Ubaya', Geofrey Kiggi, Dickson Daudi, Baraka Majogoro, Ally Yussuf, Abal Kassim Khamis/Awadh Juma dk73, Kelvin Sabato, Riphat Msuya/Haroun Chanongo dk66 na George Makang'a.
CHANZO - BINZUBEIRY BLOG
Social Plugin