Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Ojung'u Salekwa, akihutubia wajumbe wa Baraza la Madiwani, wakati wa kuhitimisha mkutano wa Baraza la Madiwani wa kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili mwaka wa fedh 2020/2021, mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Na Woinde Shizza , Arusha
Halmashauri ya Arusha imejipanga kutoa elimu ya umuhimu wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa wajibu huo wa kulipa kodi .
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ojung'u Salekwa wakati wakiongea na waandishi wa habari leo ofisini kwake kuhusiana na mikakati ya namna gani wamejipanga kukusanya mapato ya halmashauri ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wadanganyifu wamekuwa wanachukuwa vitambulisho vya machinga ili kukwepa kukadiriwa kodi inayostaili,hali iliosababisha halmashauri hiyo kutofikia lengo la ukusanyaji wa mapato kwa Kota ya kwanza ya bajeti ya mwaka 2020/2021.
Ojung'u alisema kuwa halmashauri imejipanga kutumia watalam wa ndani kutembelea biashara za wafanyabiashara hao na kubaini maeneo ya wafanyabiashara wakubwa ili kuweza kuwakadiria mapato yanayo staili na kuwathibiti wasiweze kuchukuwa vitambulisho vya machinga pindi vitambulisho hivyo vilivyoboreshwa vitakap fika na kuanza kugawiwa.
"Tunashirikiana na mkurugenzi pamoja na wataalam wetu kuwaelewesha na kuwaelimisha umuhimu wa kulipa kodi kwani wanapolipa kodi ni kwafaida yao ,kwani kodi hizo ndizo zinazotumika kuleta Maendeleo ya nchi ikiwemo kujengea barabara na vituo vya afya pamoja na huduma zingine za kijamii", alibainisha Ojung'u.
Aliongeza kuwa wanasubiri vitambulisho vipya vya machinga vilivyoboreshwa na kuhakikisha kuwa watakao pewa ni wamachinga halisi na sio wafanyabiashara wanaokwepa kodi ,huku alibainisha kuwa iwapo mfanyabiashara yeyote atakae danganya na kuchukuwa kitambulisho icho bila Vigezo hatua kali zinachukuliwa dhidi yake.
"Na nipende kusisitiza baada ya elimu tunayotoa,vitambulisho vikianza kutolewa tukamkuta mfanyabiashara mkubwa ambaye anamtaji mkubwa anakitambulisho Cha machinga Kama leseni yake atutamfumbia macho tutamchukulia hatua kali za kisheria",alisema Ojung'u.
Aidha alifafanua kuwa mapato ndiyo roho ya halmashauri ambapo alibainisha kuna maeneo wamewaondoa baadhi ya mawakala kutokana na kuihibia serikali na wakaamua kuwaweka wanajeshi wa jkt suma jambo ambalo limeshaonyesha matokeo chanya kwa muda mchache.