Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BUNGE LAAHIRISHWA HADI MACHI 30 MWAKA HUU


 Mkutano wa pili wa Bunge la 12 ulioanza Februari 2, 2021 jijini Dodoma umeahirishwa leo Februari 13, 2021 na waziri Mkuu Kassima Majaliwa hadi Machi 30 mwaka huu.

Awali ilitarajiwa kuwa vikao hivyo vingemalizika jana, lakini ilishindikana baada ya shughuli za bunge kuahirishwa kufuatia kifo cha Mbunge wa Muhambwe, Atashasta Nditiye, aliyefariki kwa ajali ya gari.

Katika mkutano huo, shughuli mbalimbali zimefanyika ambapo ulianza kwa kuwatambulisha wabunge watano walioteuliwa na Rais ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa kwanza. Wabunge wanne kutoka ACT Wazalendo na wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Aidha, wastani wa maswali 125 ya kawaida na maswali 16 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yameulizwa.

Wabunge pia walipata fursa ya kujadili Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Ufunguzi Rasmi wa Bunge la 12.

Katika hatua nyingine, bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango ili kujadili na kushauri kuhusu ‘Mapendekezo ya Mpango wa Taifa’ unaokusudiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Katika hotuba yake ya kuahirisha bunge, Waziri Mkuuu ameeleza mambo mbalimbali ambayo serikali imefanya na inaendelea kufanya ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Pia, ametumia nafasi hiyo kuzipongeza timu za taifa na vilabu vya Tanzania kwa mafanikio zilizopata kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com