WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wote wa Serikali wahakikishe wanawafikia wananchi kwenye maeneo yao, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
“Tunapaswa kuwajibika kwao badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu wa Kitaifa. Natumia fursa hii kuwaambia viongozi na watendaji wote wa Serikali kuwa tutapima utendaji wenu kwa namna mnavyotatua kero za wananchi kwenye maeneo yenu. ”
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 5, 2021) wakati akihitimisha hoja ya kujadili hotuba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa bunge la 12 Novemba 13, 2020. Amesema watendaji hao wana wajibu kwa wananchi kutokana na dhamana waliyowapatia.
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa kila mtendaji Serikalini ahakikishe anatimiza wajibu wake kikamilifu na Serikali kwa upande wake itahakikisha inachukua hatua dhidi ya wote watakaokiuka sheria, kanuni na taratibu za kazi na kamwe haitomvumilia mtumishi mzembe na mwenye kufanya kazi kwa mazoea.
Amesema nchi imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuandaa mipango na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali vya Serikali vyenye lengo la kuwaletea maendeleo wananchi, hata hivyo, awali kulikuwa na changamoto ya baadhi ya viongozi na watendaji kutowajibika ipasavyo kwa wananchi.
Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano ilijikita katika kuhakikisha inarejesha nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa kuweka mkazo katika misingi ya uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wote wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji kazi Serikalini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wabunge kwamba maoni na hoja zao zitazingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali.
Amesema kuhusu miradi inayoendelea kutekelezwa nchini katika sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, mifugo, maliasili, madini na sekta za huduma ya jamii, kama vile elimu na afya nayo itakamilishwa kama ilivyokusudiwa.