Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDAKI : MAWAKALA WANAOTUMIWA NA WAZALISHAJI WA VIFARANGA VYA KUKU WAKAMATWE KAMA HAWAJASAJILIWA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza na wauzaji wa kuku wa nyama na wazalishaji wa vifaranga baada ya kuwakutanisha na kueleza changamoto zao.Kikao hicho kimefanyika leo katika ofisi za wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Bodi ya Nyama Bw.Imani Sichwale akizungumza na wafanyabiashara wa kuku wa nyama pamoja na wazalishaji wa vifaranga vya kuku. Kikao hicho kimefanyika leo katika ofisi za wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM


Chama cha wafugaji wa kuku wa nyama TABROFA kimetakiwa kuwa na ushirikiano wa kutosha ili kuweza kutokomeza changamoto wanazozipata wafanyabiashara wa kuku hasa Mawakala wasiotambulika wanaouza vifaranga vya kuku wa nyama pamoja na vyakula vya kuku katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa Wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wa nyama Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amesema mawakala wanaotumiwa na wenye viwanda vya kutotolesha vifaranga kama hawajasajiliwa wakamatwe.

"Kuanzia sasa mawakala wa wauzaji wa vifaranga vya kuku pamoja na chakula cha kuku nataka wafuatiliwe na waeleze wapi walisajiliwa". Amesema Mhe.Ndaki.

Aidha, Mhe.Mashimba amewataka wafugaji wote wanaouza kuku wa nyama kujisajili Bodi ya Nyama kwa ajili ya biashara kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekaidi.

Pamoja na hayo Mhe.Ndaki amesema sekta ya ufugaji ni muhimu kwa pato ya nchi na kuwataka wataalamu wa mifugo kufanya tafiti za mifugo kwa kuwalenga wafugaji wenyewe kwa kubaini changamoto zao sio kuwatumia wasomi.

“Tuache kufanya tafiti kwa kuwatumia bwanashamba na bibishamba ambao hawafikishi ujumbe kwa wafugaji kuhusu elimu dhidi ya tafiti zilizofanyika,” ameeleza.

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Bw.Imani Sichwale aliwataka wafugaji hao kuacha kufuga kuku kwa mazoea bali wafuge kitaalamu kwa kuweka bajeti ya ufugaji kwa lengo la kukuza tasnia yao.

Hata hivyo Sichwale amesema kuwa nyama inasoko nje ya nchi kuliko kuku kwa sababu haijapata vigezo vya uuzaji wa nje ya nchi.

Vilevile Bw.Sichwale amesema asilimia 80 ya wafugaji wa kuku wa nyama ni wanawake hivyo amewataka kushikilia tasnia hiyo kwa lengo la kuondoa umaskini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafugaji wa kuku wa nyama TABROFA Bw.Costa Mrema amesema katika tafiti walizozifanya zimebaini kuwa ulaji wa kuku wa nyama Tanzania ni kati ya kuku laki 9 hadi milioni 1.2 kwa wiki.

"Idadi hiyo 70% ya walaji wa kuku wa nyama ni Dar es Salaam na Pwani ikifuatiwa na mikoa ya Arusha, Mwanza,Kilimanjaro na Dodoma". Amesema Bw.Mrema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com