Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWALIMU AFUKUZWA KAZI NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA WIZI WA MITIHANI


 TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, imemfikisha Mahakamani mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Orkitikiti, Kijiji cha Engong’ongare Wilayani Kiteto, Oscar Waluye na kusomewa mashtaka ya udanganyifu wa mtihani.


Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Alli Sadiki Hajji akizungumza na waandishi wa habari amesema  pia, mwalimu huyo Waluye, amefukuzwa kazi na mamlaka yake ya nidhamu.


Hajji amesema Waluye ameshtakiwa kwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba iliyofanyika Oktoba 2020 kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 23 na 24 (1) sheria ya baraza la mitihani la Taifa.


Amesema kesi hiyo ya jinai imefikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa wa mahakama ya wilaya ya Kiteto, Joakim Mwakyolo na mwendesha mashtaka wa polisi Wilfred John.


“Hata hivyo, amekana shtaka hilo na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kupelekwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Februari 16 mwaka huu,” amesema Hajji.


Amesema uchunguzi wa TAKUKURU Wilayani Kiteto umeonyesha kwamba Waluye aliwalazimisha wanafunzi wawili wa darasa la sita wa shule hiyo kufanya mitihani ya darasa la saba badala ya watahiniwa ambao uwezo wao darasani unaelezwa ni wa kiwango cha chini.


“Pia Waluye alimkaririsha mwanafunzi mmoja aliyehitimu shuleni japo mwaka 2019,” amesema Hajji.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com