Na Hellen Mtereko Mwanza
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amewataka wananchi kuweka utaratibu wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini na siyo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi.
Ametoa wito huo leo Februari 25, 2021 kwenye kikao cha pili cha bodi ya barabara ya mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika jijini Mwanza.
Alisema ni vyema kila mtu atembelee vivutio vilivyopo nchini kwa kufanya utalii kwenye hifadhi na mbuga zilizopo ili kuweza kujionea wanyama wa aina mbalimbali.
Alisema Watanzania wanapaswa kuwa wazalendo kwa kupenda vivutio vyao kwa kuvitangaza kila sehemu kwani kuanzia mwaka 1993 kulikuwa na watalii waliokuwa wakiingia kwenye hifadhi zetu 230000 ambapo mwaka 2019 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia Milioni 1.5.
"Watanzania tupo wengi kwa sasa lakini ukiangalia idadi ya watu wanaoingia kwenye hifadhi zetu na kuangalia utalii ni wachache kuliko idadi ya watu waliopo nchini hali hii inaonyesha sisi siyo wazalendo ni vyema tupende utalii wa kwetu wa ndani .Tunaendelea kuhamasisha watu wafanye utalii wa ndani ni lazima tupende vyetu vya ndani",alieleza
Ameongeza kuwa kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa kutangaza vivutio kwenye mtandao kupokea watalii kutoka ndani na nje kwani kufanya hivyo kutapelekea kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Tuna mpango wa kuanzisha utalii wa majini ambao utatumia Ziwa Victoria kwa kutumia meli, watakuwa wakitoka Serengeti watapita Saa Nane kwenda Kisiwa cha Lubondo, watakuwa na uwezo wa kwenda Chato. Halii hii itasaidia kutangaza hifadhi ya Buligi Chato na tunawahamasisha wafanya biashara kuandaa pakeji ili itakapokuwa tayari watalii watapita maeneo hayo na kuona utalii wa majini na wa nchi kavu",alisema.
Hata hivyo alisema kutokana na barabara kuchangia kwa asilimia kubwa ongezeko la watalii nchini ni vyema wakala wa barabara vijijini na mjini (TARURA) kuona umuhimu kuzitengeneza ili kusaidia kupitika kwa urahisi.
"Barabara zilikiwa hazijatengenezwa vizuri inakuwa changamoto kupitika ni vyema Wakala wa Barabara vijijini na mjini (TARURA) kuona umuhimu wa kizitengeneza na ikiwezekana kuongeza bajeti ili kusaidia kwenye matengenezo hayo na ziweze kupitika na zitasaidia kuvutia watalii na kufika eneo husikakwa urahisi na kwa wakati,",alisema Masanja.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA mkoa wa Mwanza Mhandisi Mohamed Muanda alisema kutokana na bajeti iliyotolewa watahakikisha wanarekebisha Barabara hizo hususani maeneo korofi ili zisaidie katika kutangaza utalii.
Social Plugin