Na Kadama Malunde- Malunde 1 blog
Mvua
iliyoambatana na mawe iliyonyesha kwa takribani dakika 45 kuanzia saa tisa
alasiri leo Jumamosi Februari 13,2021 Mjini Shinyanga imesababisha mafuriko na kukata mawasiliano katika
baadhi ya maeneo likiwemo eneo la kutoka Ibinzamata kwenda Kitangiri.
Maeneo
mengine yaliyoathirika ni Mtaa wa Viwandani, Mnara wa Voda na maeneo ya masoko ambapo maji yameririka kwa wingi kuingia kwenye nyumba za watu yakiwemo maeneo ya biashara na kusababisha uharibifu wa mali mbalimbali.
Malunde 1
blog imefika katika eneo la vivuko/madaraja ya kutoka Ibinzamata kwenda
Kitangiri ambapo wananchi wameonekana wakihangaika kuvuka na wengine
wakilalamika vibanda vyao kusombwa na maji.
Wananchi
wamesema mafuriko hayo yamesababishwa na miundombinu mibovu ya barabara ambapo
kuna madaraja na makalavati madogo yaliyoharibika pamoja na mitaro kuziba hivyo kusababisha maji yashindwe kupita.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila amesema tatizo la mafuriko katika
manispaa hiyo linasababishwa na ubovu wa miundombinu ikiwemo mitaro na
makalavati ya kupitishia maji akibainisha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni maeneo
yenye tatizo la mito.
“Hii Mvua imekuja kwa kasi hatukuitarajia, imenyesha
kwa muda mfupi ikiwa imeambatana na upepo na kusababisha maji kufurika na
kufunika madaraja na maji kuingia kwenye nyumba za watu”,amesema Nkulila.