Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFUJI AMUAPISHA ZEPHARINE GALEBA KUWA JAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI


 Rais Dkt. John Magufuli amemuapisha Zepharine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania ikiwa ni siku moja baada ya kumpandisha cheo ambapo awali alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

Akizungumza muda mfupi baada ya kumuapisha Jaji Galeba leo, Rais Magufuli amesema kuwa miongoni mwa mambo yaliyosababisha akampandisha cheo ni pamoja na uthubutu wake wa kutoa hukumu ya kesi kwa lugha ya Kiswahili.

Rais Magufuli amesema madai kuwa lugha ya Kiswahili haiwezi kutumika mahakamani kwa sababu haina misamiati ya kutosha hayana tija kwa sababu hakuna lugha yoyote duniani ambayo inajitosheleza.

“… tunashindwa kukitumia Kiswahili kwa sababu ya kukosa utashi na ujasiri. Lakini pia ni ishara ya kuendelea kwa kasumba fulani ya kupenda vitu vya nje na kudharau vya ndani,” ameeleza Rais Magufuli na kuongeza kuwa alimteua Jaji Galeba kwa sababu amekuwa na udhubutu na ujasiri wa kuandika hukumu kwa Kiswahili.

Rais amesema kuwa kushindwa kuitumia lugha hiyo kwenye masuala ya kimahakama na kisheria siyo tu kunawanyima haki wananchi, bali pia kuwaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi.

Kwa upande wa Jaji Galeba amemshukuru Rais kwa nafasi hiyo ya juu zaidi katika idara ya mahakama na amemuahidi kutenda kazi kwa bidii na kutenda haki kwa wananchi.

“Sina maneno ya kueleza namna nimepokea hii nafasi, labda niseme tu kwa ufupi kwamba nakuahidi kutumikia wananchi wa nchi hii kwa kutenda haki vile ambavyo Mungu anataka tutende haki huku duniani,” amesema Jaji Galeba.

Jaji Galeba alitoa hukumu hiyo katika kesi ya North Mara Gold Mine Ltd dhidi ya Gerald Nzumbi katika kesi ya Mapitio Na. 23 ya Mwaka 2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com