Kushoto ni mbunge wa Morogoro mjini Aziz Abood, na kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
**
Rais Dkt. John Magufuli ameshindwa kumvumilia na kisha kuanza kumsema hadharani mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Aziz Abood, kwa kushindwa kuendeleza viwanda na kutoa ajira badala yake alikopa hela na kununua mabasi ya kusafirisha wafanyakazi wake wanaofariki.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 12, 2021,mara baada ya kuzindua kiwanda cha ngozi cha aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Igunga Rostam Aziz, na kueleza kuwa anafikiria siku nyingine Rostam agombee ubunge wa jimbo la Morogoro ili kumtoa Abood.
"Ninampenda sana Abood lakini kwenye viwanda hapana na niwaombe Wizara ya Fedha na zingine, kwa sasa hivi tunaagiza mafuta ya kula nchi hii si ya kuagiza mafuta ya kula ili hali tuna alizeti, tuna karanga lakini viwanda tuliviua sisi wenyewe na Morogoro aliviuwa mbunge wenu", amesema Rais Magufuli
Aidha Rais Magufuli, ameongeza kuwa, "Abood amekaa na viwanda wee akaenda akakopa hela akanunua mabasi weee, kiwanda kinakufa weee, wafanyakazi wakawa wanakufa yeye anawabeba kwenye mabasi kwenda kuwazika hii siyo sawa, ninazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu".