RAIS MAGUFULI AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUTOA TAARIFA


Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watendaji wa Serikali kutoa taarifa za utendaji wa Serikali katika maeneo yao, sambamba na vyombo vya habari kutoandika habari zisizo za ukweli.

Rais Magufuli, ameyasema hayo leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua ofisi za kituo cha televisheni cha “Channel Ten” zilizopo katika jengo la “Jitegemee” na kuweka jiwe la msingi katika soko la Kisutu.

“Watendaji wa Serikali wawe wepesi kutoa taarifa sahihi kwa waandishi wa habari, utakuta yamefanyika mambo mazuri  lakini hayatolewe na wananchi hawayafahamu, tusiogope kukosolewa, lakini vyombo vya habari toeni taarifa za ukweli bila kuweka chumvi, zingatieni ukweli.” Alisema Rais Magufuli

Aliongeza kuwa licha ya Wizara na Taasisi za Serikali kuwa  Wasemaji  katika ofisi hizo bado kumekuwepo na changamoto ya utoaji taarifa kwa waandishi wa habari, na hivyo amewataka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abasi kufuatilia suala hilo.

Rais Magufuli alisema kuwa watanzania wanatakiwa kuwa wazalendo  licha ya Tanzania kuwa mojawapo wa nchi zenye vyombo vingi vya habari duniani ambapo mwaka 2015 kulikuwa na vituo 106 vya redio vilivyosajiliwa, vituo vya televisheni 25, ambapo Februari 2021, kumekuwepo na vituo vya redio vilivyosajiliwa 195 na vituo vya televisheni 46. Pamoja na redio za mtandaoni 23 na televisheni za mtandaoni 440 na magazeti na majarida 247 vimesajiliwa hadi kufikia Februari 2021.

“Vyombo vya habari mnajitahidi kutoa habari, lakini mtangulize sana uzalendo na hakikwa yule anayeandikiwa habari, kumekuwepo na uzushi sana mara fulani kafa ni mambo ya ajabu” alisema Rais Magufuli

Alisisitiza “Lakini pia katika habari ambazo taifa letu linaandikwa vibaya watu wanashabikia, uzalendo umepungua tutangulize uzalendo wa nchi yetu, niwaombe watanzania wetu tutangulize maslahi ya taifa, wajenga nchi ni sisi na wabomoa nchi ni sisi.”



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post