SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI KUZUIA UKEKETAJI NCHINI
السبت, فبراير 06, 2021
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema Serikali inaendelea kushirikiana na Wadau kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukeketaji wa watoto wa kike nchini.
Taarifa hiyo ya Dkt. Jingu imetolewa leo kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sebastian Kitiku mbele ya Waandishi wa Habari, katika kuadhimisha siku ya Kimataifa kupinga Ukeketaji.
Amesema pamoja na mikakati iliyopo ya kisera na kisheria, Wizara inatarajia kuzindua mkakati wa kutokomeza ukeketaji wa mwaka 2019-2022 utakaohakikisha ngazi zote za jamii zinashiriki katika kutokomeza vitendo hivyo.
Aidha amesema Serikali inaendelea kuimarisha maeneo ya mipaka ya nchi kwa kuzijengea uwezo Kamati za Usalama za Wilaya ili kuzuia ukeketaji unaofanywa kwa kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Akibainisha hali ya ukeketaji nchini amesema katika wanawake 10, mmoja amekeketwa huku Mikoa ya Manyara, Dodoma, Arusha, Mara na Singida ndiyo inaongoza kuendeleza vitendo hivyo kutokana na mila na desturi potofu, ikiwemo imani kuwaponya na magonjwa ya mfumo wa mkojo.
“Ukeketaji una athari kubwa kwa wanawake na watoto wa kike kijamii na kiafya. Athari hizo ni pamoja na kuendeleza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike, kuchochea mimba za utotoni pamoja na kutengwa na jamii” amesema Kitiku.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa kupinga Ukeketaji yanafanyika kila tarehe 06 Februari ya kila mwaka na kwa mwaka huku yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Wakati ni huu: Tuungane kupinga vitendo vya Ukatili”.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin