Kwa muda mrefu wakazi wa maeneo hayo hawakuwa na usafiri wa uhakika na hiyo iliwalazimu kutumia boti ndogo na majahazi kwa ajili ya kusafirishia mizigo na abiria na hivyo kuhatarisha maisha yao baharini endapo ingetokea dharura ya ajali.
Kivuko hicho kipya kilichogharimu shilingi Bilioni 5.3 mpaka kukamilika kwake na ambacho ujenzi wake umegharamiwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani, kimejengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza katika karakana yake ya kujengea na kukarabati vivuko iliyopo Kigamboni jijini Dar es salaam na kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 10 ambazo ni sawa na tani 100.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea kivuko hicho iliyofanyika katika kisiwa cha Mafia na kuhudhuriwa na viongozi kadha wa kadha wa mkoa huo, mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kutoa fedha zote hizo kwa ajli ya kuhudumia wananchi wake na pia aliupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kuweza kusimamia ujenzi wa Kivuko hicho hadi kukamilika kwake.
‘’Kama mlivyosikia katika hotuba zilizotangulia Wakala umekamilisha miradi ya ujenzi wa vivuko vipya vya Kayenze – Bezi, Bugolora - Ukara na Chato – Nkome na kufanya vivuko vipya vilivyonunuliwa katika mwaka wa fedha 2019/20 kuwa vinne kikiwepo hiki cha Kilindoni tunachokipokea leo kwa pamoja vikiwa vimegharimu jumla ya Shilingi bilioni 15.3. Haya yote ni matunda ya kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Dr. John Joseph Pombe Magufuli, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’’
Alisema Mheshimiwa Ndikilo ambapo aliongeza kuwa kwa kuwa Kivuko hicho ni rasilimali muhimu ya Taifa na kinahitajiwa na wananchi wa Mafia na Nyamisati, aliuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kusimamia kwa karibu uendeshaji wake ili wananchi wafaidi matunda mazuri ya Serikali yao kwa fursa ya maendeleo yao binafsi na nchi nzima kwa ujumla wake na pia aliwasisitizia wananchi wa Mafia na Nyamisati kukitunza kivuko hicho na kuwapa ushirikiano wa kutosha wahudumu wake kiweze kuwahudumia kwa kipindi kirefu.
Naye mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga, Mhandisi Elizabeth Manzi akizungumza katika hafla hiyo, amesema ni dhamira ya Serikali kutaka kutoa huduma iliyo bora yenye kukuza uchumi wa nchi ya Tanzania na Katika mwaka wa fedha 2019/20, Serikali ilitoa jumla ya Billioni 12,245,214,800.00 kwa ajili ya miradi ya vivuko na maegesho ambayo inatekelezwa na Wakala wa Ufundi na Umeme na Fedha hizo zinatokana na Mfuko Mkuu wa Serikali na Mfuko wa Barabara.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa kivuko hicho alisema, kazi ya ujenzi huo imefanywa kulingana na viwango vinavyokubalika Kimataifa (IMO Standards).
‘’Kivuko hiki kimefanyiwa ukaguzi wa mwisho kabla ya kuanza kazi na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambao walikuwa wakishiriki ukaguzi wakati wa ujenzi ili kuthibitisha viwango vya usalama wa abiria, magari na mizigo.’’ Alisema Mhandisi Maselle ambapo aliongeza kuwa baada ya ukaguzi wa mwisho TASAC wamefanya usajili wa kivuko hiki kabla hakijaanza kazi kwa jina la MV KILINDONI – HAPA KAZI TU.
‘’Ili kuhakikisha usalama wa kivuko hiki kinapofanya kazi kimefungwa vifaa stahiki vya kuongozea kama vile Radar, GPS, Echo Sounder, vifaa vya mawasiliano (Communication equipment) na vifaa vya uokoaji vya kutosha kwa watu wazima na watoto ambavyo ni makoti ya kujiokoa (life jackets) na maboya (life rafts na life buoys).’’ Alimaliza Mtendaji Mkuu ambapo alishukuru Serikali kwa kuendelea kuuamini Wakala katika kutekeleza miradi hiyo na pia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya vivuko kwa lengo la kuboresha huduma za usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini na kuahidi kukitunza kivuko hicho kwa kukifanyia matengenezo kama inavyotakiwa ili kiweze kudumu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa wakati wote.
Kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha MV. KILINDONI HAPA KAZI TU kunafanya idadi ya vivuko kote nchini kufikia 33 hadi hivi sasa na hivyo kuifanya serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri kwa manufaa ya wananchi wengi.
Social Plugin