*****************
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesaini makubaliano na Klabu ya Simba ya kujitolea kutangaza utalii wa Tanzania kupitia nembo yao mpya ya “Visit Tanzania” waliyoizindua kwa lengo la kuongeza watalii kutoka nje ya Tanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro mara baada kusaini makubaliano hayo jijini Dodoma leo.
Amesema kwa kufanya hivyo Simba inasaidia kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka Tanzania iwe na ongezeko la idadi ya watalii, mapato yatokanayo na utalii na mazao mapya yatokanayo na utalii.
“Ni Uzalendo wa hali ya juu ambao Simba wameufanya na ninawatangaza Simba Sports Club kama mabalozi wa Utalii Tanzania kwa sababu wamejitoa na wameonesha kweli wana uwezo wa kuiwakilisha nchi sio tu uwanjani hadi nje ya uwanja” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro ameipongeza timu ya Simba kwa kujitokeza kutangaza utalii wa Tanzania na kubainisha kuwa tukio hilo ni la kwanza katika historia na kwamba timu hiyo haijalipwa chochote.
Naye, Mkurugenzi wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez amesema timu yake imeona umuhimu wa kutangaza utalii wa Tanzania kwa kuzindua nembo mpya ya ‘Visit Tanzania’.
“Tumeamua kuipeperusha Bendera ya Tanzania si tu kwenye jezi bali pia kupitia nembo hiyo tutakayoibandika kwenye mabegi, nguo za safari, kofia na barakoa na kutangazwa kupitia mitandao yetu ya kijamii” amefafanua Gonzalez.
Kwa upande wake Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara amewataka watanzania kushiriki katika kuitangaza Tanzania.
“Ni wajibu wa kila mtanzania kushiriki katika kutangaza utalii wan chi yetu” amesisitiza.
Makubaliano hayo kati ya serikali na Tanzania yamefanyika wakati timu ya Simba ikielekea kwenye hatua ya makundi katika Champion League.