Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA YA UTEKELEZAJI MAAMUZI YA SERIKALI KUHUSU MIGOGORO YA MATUMIZI YA ARDHI KATIKA VIJIJI 975 YAWASILISHWA


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvu amewaoongoza Mawaziri wenzake wa Wizara za Kisekta kupokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kuhusu Migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 vilivyopo katika hifadhi na Mapori ya Akiba.

Taarifa hiyo iliwasilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo tarehe 4 Februari 2021 jijini Dodoma kwa niaba ya Kamati ya Mawaziri na Wataalamu kutoka Wizara za Kisekta.

Wizara za kisekta zinazoshiriki ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Makamu wa Raisi, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Maji. Aidha, katika kikao hicho Wizara za Mambo ya Ndani Nchi, Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Fedha zilialikwa kutokana na umuhimu wa wizara hizo katika utekelezaji wa maamuzi.

Akizungumza wakati wa uwasilishwaji taarifa hiyo, Waziri wa Ardhi William Lukuvi  alisema, mbali na mambo mengine Taarifa ya vijiji 975 vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi itawezesha Mawaziri wa Wizara husika aliowaeleza kuwa, wengi wao ni wageni kujua mpango mkakati na namna ya utekelezaji  wa maamuzi ya Serikali kuhusiana na kunusuru vijiji 975.

‘’Hapa wengi wenu ni wageni karibu asilimia 80, hivyo taarifa inayowasilishwa leo itawasaidia kujua utekelezaji wa maamuzi ya serikali kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975’’ alisema Lukuvi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema kupitia kikao hicho kuwa, pamoja na Kamati kutekeleza maamuzi ya Serikali kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975, wizara yake imetekeleza pia baadhi ya mambo kwa lengo la kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi kama vile kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika vijiji 114 vinavyozunguka hifadhi.

Utekelezaji wa maamuzi ya Serikali kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 nchini unafuatia kukithiri kwa migogoro ya ardhi ambapo, Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari 2019 aliunda Kamati ya Mawaziri wa Kisekta chini ya Waziri wa Ardhi William Lukuvi ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Kufuatia mapendekezo ya Kamati, Baraza la Mawaziri mnamo mwezi Septemba, 2019, liliridhia kuwa vijiji 920 kati ya vijiji 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi na mapori visiondolewe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com