Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU]mkoa wa Dodoma imefanikiwa kumpata mmiliki wa kampuni Geneva Credit Shop ya Mjini Kondoa Abubakary Kinyuma ama maarufu Bwana Mapesa na kumwamuru kurejesha Tsh.Milioni mia moja sabini na sita laki tano sitini na tano elfu[176,565,000] na nyumba moja kwa walimu wastaafu 17.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 18,2021 jijini Dodoma mkuu wa TAKUKURU mkoani Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma wilayani Kondoa wanapokaribia kustaafu huchukua mikopo midogo kwa Bw.Mapesa ambaye amekuwa akichukua kadi zao za benki na kuzihifadhi na pindi mafao yao yanapotoka hujitwalia kiasi kikubwa cha fedha kwa riba kubwa hadi kufikia asilimia elfu kumi.
“Mwezi uliopita [Januari 2021 ]tuliwatangazia kuwa tunafanya uchunguzi dhidi ya kampuni ya ya Geneva Credit Shop ya mjini Kondoa inayojihusisha na ukopeshaji wa fedha ,baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wengi ambao wanadai kupatiwa mikopo umiza na kampuni hiyo na uchunguzi wetu ulibaini kuwa walilipishwa fedha hizo za mafao na kunyang’anywa na Bw. Mapesa kinyume na taratibu",amesema.
Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma amesema mwalimu mstaafu mmoja alikopeshwa Tsh. Laki tatu na elfu hamsini [350,000/=] pamoja na kurejesha Tsh. Milioni nne na laki sita[4,600,000=/] pia alinyang’anywa nyumba yenye yenye thamani ya Tsh.Milioni thelathini na saba[37,000,000/=] iliyopo kiwanja Namba 115 kitalu C eneo la Ndachi East jijini Dodoma.
Bw.Kibwengo ameainisha baadhi ya malipo yaliyofanyika leo kwa wastaafu ni pamoja na Juma Hindo aliyerejeshewa Tsh.Milioni ishirini na saba na laki nne na themanini na nane elfu[27,488,000/=],Ayub Bakari aliyepatiwa Milioni ishirini na tatu na laki nne[23,800,000/=],Ally Tarimo milioni kumi na nne laki moja na nusu[11,150,000/=],huku fedha zingine zilizorejeshwa ni Tsh.milioni ishirini na tatu na laki nne[23,400,000/=], pamoja na Tsh.Milioni kumi na sita na laki nane[16,800,000/=].
Aidha,Bw.Kibwengo ameendelea kufafanua kuwa kwa kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania[TRA] TAKUKURU inaendelea kukokotoa kiasi cha kodi ambacho kampuni hiyo ya ukopeshaji inadaiwa na kuendelea kufuatilia Tsh.Milioni mia moja themanini na nne laki tano themanini na sita [184,586,000/=]za wakopeshwaji 22 ambazo pia zinapaswa kurejeshwa na BW.Mapesa.
Katika hatua nyingine Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU imemrejeshea Bw.Dismas Kweka ,mfanyabiashara na mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma Tsh.milioni tano [5,000,000/=],
“Ufuatiliaji wetu umewezesha kuziokoa kutoka kwa Bw.Richard Mwambenje ambapo Disemba 2021 tulimrejeshea Bw.Kweka ambaye aliuziwa kiwanja Na.18 kwa Tsh. Milioni tisa na laki saba[9,700,000/=] na leo anapatiwa kilichosalia kiwanja hicho kilitolewa na mwananchi mmoja kama sadaka kwa Jumuiya ya Uamsho wa Wakristo Tanzania [UWATA] lakini Bw.Mwambenje ambaye alikuwa katibu wa UWATA alikiuza kwa kutumia mkataba wa kughushi”amesema .
Pia,Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani Dodoma Bw.Kibwengo amebainisha kuwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imefanikiwa kurejesha deni la Tsh.milioni hamsini na moja laki sita sabini na nane elfu na mia saba thelathini na tatu[51,678,733/=] kwa chama cha akiba na kukopa cha Ufundi SACCOS baada ya kuwabana wanachama ambao ni wadaiwa sugu wa muda mrefu.
Hivyo,Bw.Kibwengo ametoa wito kwa wakopeshaji wa fedha mkoani Dodoma kuzingatia sheria ,kanuni na taratibu za nchi na kuacha na kuacha kuwatoza wananchi riba umiza huku pia akiwaasa wananchi kujihadhari na mikopo umiza na kutokubali kukabidhi kadi zao za benki kwa mtu yeyote.
Kwa upande wao baadhi ya walimu wastaafu akiwemo Mwalimu Juma Hindo na Mwalimu Halima Tarimo wameipongeza TAKUKURU kwa kuendelea kutetea Wanyongo ambapo mwalimu Hingo amesema alikopa Tsh. Laki mbili baada ya kustaafu aliamuliwa kulipa riba ya Tsh,milioni 30.
“Bado huyu ndugu yetu anazidi kuumiza wanyonge mwaka 2014 nikiwa kazini nilikopa Tsh.laki mbili baada ya kustaafu mwaka 2017 Mzee Mapesa alikuja na mgambo wake wawili walileta bili ya Tsh.Milioni 30 mimi sikuwa na pesa maana pesa zote zilikuwa benki na nilikuwa na trekta niliuza kwa Tsh.Milioni 16 na nikaenda benki kutoa milioni 14 Jumla nikampa milioni 30”,amesema.