Bakari Harith Mwapachu, wakati wa uhai wake
***
Aliyewahi kuwa mbunge wa Tanga na Waziri wa Sheria na Katiba Bakari Harith Mwapachu, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Februari 12, 2021, katika hospitali ya Taifa Muhimbili, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mwapachu alikuwa mbunge wa Tanga kuanzia 2000 hadi 2010 na amewahi kushika nafasi mbalimbali Serikalini kwa nyakati tofauti.
Spika wa Bunge mstaafu Mzee Pius Msekwa na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, wamesema kuwa marehemu Bakari Mwapachu alikuwa ni mchapakazi na mtu makini katika kazi zake.
"Mwapachu alikuwa ni mtu makini sana katika kazi zake na katika ubunge alikuwa amakini sana katika kusimamia jimbo lake na katika Uwaziri wake alikuwa ni mtu wa kujenga hoja Bungeni kiasi cha kuwaridhisha wabunge na kubwa la kujifunza kwa mtu yeyote aliyekutangulia ni ule uadilifu katika utendaji wake wa kazi", amesema Mzee Msekwa
Kwa upande wake waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amesema kuwa, "Mwapachu nimefanya naye kazi lakini siyo tu kazi lakini alikuwa ni rafiki yangu sana na familia zetu zilikuwa zinatemnbeleana alikuwa ni mzee wa busara sana na alikuwa hana papara, Taifa limepoteza hazina kubwa"
Bakari Harith Mwapachu, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Februari 12, 2021, katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.