Kiongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu ametoa salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika ukurasa wake wa Twitter Lissu amesema Maalim Seif alikuwa kiongozi mwenye ushawishi, na mtetezi wa Wazanzibari asiye na woga.
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Maalim Seif amekuwa nguzo muhimu ya ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi katika taifa la Tanzania na mtetezi mkubwa wa maslahi ya Zanzibar.
Zitto ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya msiba wa Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha ACT-Wazalendo kwa Umma wa Watanzania.
''Ninajua kifo cha Maalim Seif kitawashtua na kuwafadhaisha wanachama wa ACT, Wazanzibari na Watanzania, ninapenda kuwahakikishia kuwa tutayaenzi maono yake aliyoyaishi wakati wa uhai wake''.
Amewataka Wazanzibari na Wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania kwa ujumla wawe na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright amesema ni kiongozi aliwaweka watu wake mbele kwanza kabla ya madaraka.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein kufuatia kifo cha Makamu wake wa Kwanza wa Rais Mhe. Seif Sharif Hamad.
Ikulu ya Kenya imeandika katika ukurasa wa twitter alikuwa kiongozi maarufu, mwenye busara na maendeleo na mchango wake kwa watu wake na ukanda wa Afrika Mashariki utakumbukwa.